TANZANIA inaendelea kupiga hatua kwenye sekta ya elimu kwa kuweka mikakati mingi mfano; kuanzisha, kuongeza shule za msingi na sekondari, kugharamia elimu kuanzia msingi hadi sekondari na kujenga shule za sayansi kwa wasichana.
Moja ya malengo ya kuwekwa kwa mikakati hiyo ni kutaka kila mtoto awe wa kutoka familia maskini au tajiri, apate elimu.
Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba elimu ndio msingi mkuu wa kumwezesha mtu kuwa na uelewa wa kutosha, kwani elimu ndio inayomfanya aweze kujitambua na kujimiliki mwenyewe.
Vilevile, elimu inamfanya mtu aweze kuzikabili changamoto zinazomzunguka katika maisha yake ya kila siku na pia kuweza kuyatawala na kuyatumia mazingira yake ili kuboresha maisha yake.
Hata hivyo, kumekuwapo na wingi wa mimba za wanafunzi na ndoa za utotoni kwa kwenye baadhi ya maeneo ambazo kwa namna moja au nyingine ni kikwazo kwa maendeleo yao kielimu kwa watoto wa kike.
Kwa mfano, ndani ya mwezi mmoja wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 194 walibainika kupewa mimba na kukatishwa masomo yao katika wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo, wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Chiwanda wilayani humo hivi karibuni na kuwataka wazazi na walezi kutomalizana kimya na wahalifu.
Wilaya moja idadi ya wanafunzi waliopata mimba ndani ya mwezi mmoja ndio hiyo. Idadi kama ikiwa katika kila wilaya kwa nchi nzima yenye wilaya zaidi ya 100 hali itakuaje?
Ipo haja kwa jamii kulinda maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike kwa kushirikiana na serikali kukikabiliana na tatizo la mimba hizo, ambazo zimekuwa ni kikwao cha maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike.
Mimba zinasababisha upatikanaji wa elimu kwa wote kukabiliwa na tatizo na huenda linazidi kuwa kubwa iwapo jamii itajiweka pembeni kwenye vita hiyo ya kutokomeza ukatili huo wa kijinsia.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, maofisa elimu na ustawi wa jamii wajitahidi kuwa wabunifu kwa kuanzisha klabu rika, katika shule na kwa shule ambazo klabu hizo zipo, basi ziimarishwe.
Ikumbukwe kuwa wasichana wanaokatisha masomo na uharibu maisha yao, wamo ndani ya jamii na ni sehemu ya jamii, hivyo ni muhimu jamii ihusike katika kukomesha mimba na ndoa za utotoni.
Wazazi na walezi nao hawana budi kuzungumza na watoto wao na kuwaelekeza, kuwafundisha maadili mema wakiwa wadogo ili yawe ngao yao ingawa inawezekana wakayaacha, lakini ni muhimu kutimiza wajibu katika malezi.
Elimu ya makuzi ni ya muhimu, kwani ni mojawapo ya njia ya kuwaepusha tamaa, ambazo mwisho wake zinaweza kusababisha wapate mimba na kukatisha masomo bila kutarajia.
Suala la malezi pia linawagusa walimu, kwani wao ndio wanaokaa na wanafunzi muda mrefu na wanaona mabadiliko ya wanafunzi kitaaluma, kitabia, kimwenendo na kimaadili.
Walimu wasiwe sehemu ya tatizo la mimba, kwani baadhi yao huwa wanatuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao, kitendo ambacho kinaonyesha kuna mmomonyoko wa maadili.
Kwa ujumla ni kwamba kila atakayebainika kujihusisha na mapenzi na wanafunzi, sheria ichkue mkondo wake bila kujali ni nani. Awe mwalimu, ndugu wa mwanafunzi au mtu yeyote, wote wanapaswa kuchukulia hatua za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii.
Wanafunzi wa kike kama walivyo wa kiume, nao wana ndoto zao walizojiwekea katika elimu, hivyo kuwapa mimba ni sawa na kuwaharibia ndoto hizo hata kama kwa sasa kuna utaratibu wa wao kurudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED