KenGold itaweza kumdhibiti 'chautundu' Morrison atulie?

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:42 AM Feb 03 2025
Bernard Morrison.
Picha: Mtandao
Bernard Morrison.

KUTAMBULISHWA kwa Bernard Morrison KenGold FC, hilo ni jambo moja, je inaweza kumdhibiti 'chautundu' huyo?

Hili ndilo jambo linaloulizwa na kusubiriwa na mashabiki wengi wa soka nchini. Ni baada ya winga huyo raia wa Ghana, kujiunga na timu hiyo kwa wachezaji waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Kinachowafanya mashabiki wengi waulizane na kufikiria hivyo ni tabia ya utundu aliyonayo mchezaji huyo licha ya kuwa na kipaji kikubwa cha kusakata kabumbu.

Mwenyewe amebainisha kuwa hajaenda KenGold kutafuta pesa, kwani angeweza kuzipata kwa kujiunga na timu zingine kubwa. Morrison hata kama yeye mwenyewe hajasema, lakini kila mmoja anajua kuwa anaweza kuichezea timu yoyote kubwa hapa nchini kutokana na uwezo wake.

Anasema ameamua kuichezea KenGold, kwa sababu anahitaji kucheza bila presha ili kujiweka sawa kimwili, na kiakili kwenye timu ambazo hazina mahitaji makubwa tofauti na angeenda timu nyingine, kwani ndiyo kwanza ametoka kwenye chumba cha majeruhi kujiuguza kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa na Klabu ya FAR Rabat ya Morocco.

Akasema kuwa KenGold ipo ndani ya uwezo wake, kwani ni timu ambayo haiitaji mambo mengi zaidi ya kutaka kubaki tu Ligi Kuu, kitu ambacho anaweza kukifanikisha kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.

Akiwa hapa nchini, Morrison alizichezea Klabu za Simba na Yanga, lakini kote huko amekuwa haishiwi na vituko, kiasi cha kuwa gumzo sana nje ya uwanja kuliko ndani.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa alikuwa akicheza vema mechi chache sana kwa uwezo wa hali ya juu kiasi cha kila mmoja kukubali uwezo na kipaji ambacho amejaaliwa kuwa nacho.

Kwa msimu mzima anaweza kuamua kucheza mechi tatu tu au nne kwa kiwango cha hali ya juu, lakini zingine zote akawa wa kawaida tu.

Na alifanya hivyo akiwa kwenye klabu kubwa zenye mashabiki wengi, hivyo wasiwasi wangu na baadhi ya mashabiki itakuwaje kwenye timu ndogo kama hiyo?

Kama alikuwa akiwapelekesha viongozi wa timu kubwa, viongozi wa KenGold wanaweza kumdhititi?

Wasiwasi wangu mwingine ni kwamba, KenGold, ambayo mbali ya kuwa ni ndogo, haipo Dar es Salaam, ambako ndiko hupenda zaidi kuishi, je anaweza kuishi Chunya bila kuomba ruhusa za mara kwa mara za kwenda Dar es Salaam?

Taarifa kutoka kwa watu wa  Simba na Yanga zinasema, alikuwa na tabia ya kuondoka kambini wakati mwingine bila ruhusa, kitu ambacho kilikuwa kikiwakasirisha viongozi wa timu hizo na kushindwa kuishi naye kwenye mazingira kama hayo.

Labda kama mwenyewe ameamua kubadilika, kwani wakati mwingine muda ni mwalimu mzuri, inawezekana kabisa Morrison huyu siyo yule ambaye tunamfikiria na huenda amejifunza kutokana na makosa ya mwanzo na sasa ameamua kutulia.

Lakini kama atakuwa yule yule basi viongozi wa KenGold watafanya kazi ile ile ambayo ilikuwa ikiwakumba viongozi wa Simba na Yanga.

Inawezekana wao wakawa na dawa ya kumtuliza na kumfanya aelekeze nguvu zake uwanjani zaidi, pia uwezo wake uonekane kwenye michezo yote na si baadhi tu ambayo yeye mwenyewe inawezekana anaamua afanye kweli. 

Kama Morrison akiamua kukipiga kweli na kuacha utukutu, hakuna winga yeyote nchini anaweza kufikia uwezo wake. Nafikiri pia kama Morrison akiwa kwenye kiwango kile ambacho kila mmoja anakifahamu, akiachana na 'utukutu', sidhani kama baada ya msimu ataendelea kuwa hapo.

Alijiunga na Yanga kipindi cha dirisha dogo la usajili 2020, na alipomaliza miezi yake sita, akatimkia Simba alipocheza kwa misimu miwili hadi 2022, akarejea tena Yanga, ambako alikipiga kwa msimu mmoja tu hadi 2023, akachukuliwa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, wakati huo, Nasreddine Nabi, kwenda katika timu aliyoenda kuifundisha, FAR Rabat ya Morocco.