Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemjibu Rais wa Marekani wa wakati huo, Donald Trump, baada ya Trump kutangaza kusitisha misaada kwa taifa hilo akidai kuwa kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na madai kuwa Wazungu wananyanyaswa na kupokonywa ardhi wanazomiliki.
Akijibu madai hayo, Ramaphosa amemtaka Trump aache kuingilia masuala ya ndani ya Afrika Kusini kwa kuwa hayamhusu. Amesisitiza kuwa ardhi ya Afrika Kusini ni ya raia wa nchi hiyo, na Trump hana mamlaka ya kuwapangia cha kufanya.
“Hii ni ardhi yetu, sijui Donald Trump anahusika vipi au atafanya nini kuhusu ardhi ya Afrika Kusini kwa sababu hajawahi kuwa hapa. Aitunze Marekani yake, nasi tutaitunza Afrika Kusini yetu. Afrika Kusini ni ardhi yetu na inamilikiwa na watu wote wanaoishi hapa, siyo ya Trump,” amesema Ramaphosa.
Aidha, Ramaphosa ameeleza kutoridhishwa na kile alichokiita upendeleo wa Trump katika masuala ya kimataifa.
“Nikikutana na Trump, nitamwambia wazi kuwa yeye ni mtu mbaya kwa sababu anapendelea upande mmoja. Marekani ilikuwa na wenyeji wa asili ambao waliwafukuza na kuwaangamiza karibu wote. Sisi hapa tunaishi kama taifa lenye watu weusi na weupe, na tunatafuta suluhisho sisi wenyewe kuhusu suala la ardhi. Trump atuache, atuache kabisa,” amesisitiza.
Ramaphosa pia amemkumbusha Trump kuwa wakati wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Marekani haikushiriki moja kwa moja katika kupigania ukombozi wa taifa hilo.
“Wakati sisi tunakandamizwa na kunyanyaswa na utawala wa Makaburu, Trump hakuwepo hapa. Hakupigana bega kwa bega nasi, na sisi wenyewe tulitatua tatizo hilo kwa msaada wa watu wengine duniani. Trump aendelee na mambo yake huko White House, nasi tutaendelea na mambo yetu hapa. Pambana na mambo yako, nasi hatutaingilia mambo ya Marekani,” amesema Ramaphosa kwa msisitizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED