VIJANA wawili wakazi wa Kijiji cha Remagwe Kata ya Regicheri Tarafa ya Inchugu wilayani Tarime mkoani Mara wameuawa kwa kukatwa mapanga na Wananchi wenye hasira kali wakiwatuhumu kumvamia Sofia Werema kisha kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili hadi utumbo kutoka nje.
Vijana hao ni pamoja na Nyamhanga Mrimi (28) na Moris Gokoya (26) ambao wanadaiwa kukodiwa kufanya uhalifu huo huku anayesadikiwa kuwakodi akitokomea kusikojulikana.
Akielezea tukio hilo jana, Diwani wa Kata hiyo ya Regicheri Mbusiro alisema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki na kuwa vijana hao walishambuliwa wakituhumia kumchoma visu Mwanamke huyo.
Alisema Mwanamke huyo aliyetambuliwa kwa jina la Sofia Werema akiwa nyumbani alivamiwa na kumchoma visu sehemu mbalimbali ya mwili hadi utumbo kutoka nje ambako alikimbizwa Hoaspitali ya Dk.Stephen na kulazwa huko hadi sasa.
Alisema hali ya mama huyo bado haijaimarika vyema na kudai kuwa aliwatambua na kuwafahamu waliomvamia na kumchoma visu kisha kuwataja kwa ndugu zake.
"Ilikuwa Jumapili wananchi wakazi wa Kijiji hiki walikusanyika hapa Kijijini na kupiga Kengere na Watu wengi kujitokeza na kuanza kufanya msako kuwasaka washukiwa hao na walipohojiwa na Wananchi hao sababu za kumshambulia Mwanamke huyo walidai kuwa walikodishwa na Mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Emanuel Yusufu,"alisema Mbusiro.
Alidai kuwa Mtu huyo alikuwa na Kesi ya madai Mahakama ya Mwanzo Sirari na kuwa mama huyo aliyechomwa visu alishiriki kutoa ushahidi katika kesi hiyo hivyo lusadikiwa kukodi vijana hao wamshambulie ili kupoteza ushahidi.
Alidai baada ya Wananchi kubaini hayo walilawashambulia hadi kufa huku wakichoma mali za anayedaiwa kuwatuma vijana hao ikiwemo duka lake la dawa.
"Tunawaasa Wananchi kutojichukulia sheria mkononi badala yake kufikisha maswala yao kwenye vyombo vya sheria ili hatua zaidi ziweze kufatwa dhidi ya Watuhumiwa,"alisema Diwani huyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Remagwe Wandwi Mongora alisema tukio hilo linahusishwa na chuki na kuwa kama serikali haifurahii kuawa kwa vijana hao na kuwa wanasubiri Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya SACP Michael Njera alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi sababu za mauaji hayo.
Alisema miili imehifadhiwa Chumba cha kuhifadhi maiti kituo cha afya Sirari na inatarajiwa kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
"Tunatoa wito kwa Wananchi kuacha kujichukulia Sheria mikononi badala yake kuyafikisha malalamiko yao kwenye vyombo husika badala ya kujichukulia maamuzi kama hayo ambayo yanaleta chuki na uhasama katika Jamii," alisema Kamanda Njera.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED