MFANYABIASHARA na mdau wa Maendeleo wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Shaaban Mwanga, amemaliza changamoto ya kukosekana kwa daraja dogo la Kibohehe, liliko Kata ya Machame Romu, ambalo liliwatesa wananchi kwa kukosa kivuko hicho kwa miaka 64 sasa.
Waathirika wakuu waliokumbana na adha ya kukosekana kivuko hicho cha Korongo la Kibohehe, ni wananchi, waendesha pikipiki maarufu bodaboda na wanafunzi wa Shule za Msingi Roo, Kibohehe, Tolu na Shule ya Sekondari Kibohehe.
Akizungumza jana, alipokwenda kuzindua daraja hilo dogo lililogharimu zaidi ya Sh. milioni 4.15, Mwanga, amesema eneo hilo ambalo limeinuka, mara nyingi hasa wakati wa mvua, wananchi hupata adha kubwa ya kuvuka upande wa pili kwenda upande mwingine.
Amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo dogo, wananchi walikuwa wakitumia gharama kubwa za usafiri, usafirishaji wa mazao yao kutoka shambani na majumbani kwenda katika Soko la Kimataifa la Mazao la Kwa Sadala.
“Kubwa lililotukutanisha hapa, ni uzinduzi wa daraja letu (kivuko), ambalo baada ya kuanza ujenzi wake tarehe 6, Oktoba 2024. Eneo hili limekuwa ni korofi kama mnavyoona.
“Sio wananchi wa kawaida tu, hata waendesha pikipiki kwa maana ya bodaboda na wanafunzi, wakati wa mvua kubwa mawasiliano yanakatika kutoka eneo moja kwenda jingine na hawawezi kuendelea na safari.
…Wananchi walikaa wakaona kwamba iko haja kunishirikisha mimi kama mdau wa maendeleo, tukakaa nao tukaangalia ni jinsi gani kusaidiana kujenga hilo daraja.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED