Walimu wa Sayansi, Hisabati watakiwa kutumia teknolojia kuboresha ufundishaji

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 07:38 PM Feb 03 2025
Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Katavi, Silivano Sichone akifungua mafunzo endelevu ya Walimu kazini wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Rukwa, Songwe na Katavi, yanayofanyika shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda.
Picha: Grace Mwakalinga
Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Katavi, Silivano Sichone akifungua mafunzo endelevu ya Walimu kazini wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Rukwa, Songwe na Katavi, yanayofanyika shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda.

WALIMU wa Masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi, wametakiwa kutumia vishkwambi (tablets) na simu za mkononi za kisasa (smartphones), kama nyenzo muhimu za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wanapokuwa darasani.

Kauli hiyo imetolewa  leo na Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Katavi, Silivano Sichone, wakati wa ufunguzi wa mafunzo endelevu ya walimu kazini, wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati, yanayofanyika katika shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda iliyopo mkoani humo.

Sichone amesema  ni vyema walimu kutumia vifaa vya kisasa kama vishkwambi na simu za mkononi, kwani vifaa hivyo vitawawezesha wanafunzi kupata ufahamu mzuri wa masomo yanapowasilishwa kupitia  mada mbalimbali darasani.

Ameongeza kuwa vifaa vya kidijitali kama vishkwambi na simu za mkononi vinatoa fursa ya kutoa maelezo ya kina kupitia video, picha, na michoro ya kisayansi, ambayo mara nyingi ni vigumu kuonyeshwa kwa njia za kawaida, itawawezesha wanafunzi kuelewa na kukumbuka mada kwa urahisi zaidi.

1

"Masomo haya mara nyingi yanahitaji mifano na mazoezi ya vitendo ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji, kwa kutumia teknolojia, walimu wanaweza kutoa masomo kupitia programu za kompyuta au programu maalum zinazowawezesha wanafunzi kushiriki katika mazoezi ya mtandaoni na majaribio ya kisayansi," amesema  Sichone.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo pia yatahusisha wathibiti ubora ambao wataweza kusaidia kuboresha tathmini za walimu na kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu mada mbalimbali za kisayansi zinazofundishwa darasani.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo Kituo cha Katavi, Majaliwa Mkalawa, amesema  washiriki 675 kutoka mikoa ya Rukwa, Songwe na Katavi wanashiriki mafunzo ya masomo ya Sayansi, Hisabati, pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika ufundishaji na ujifunzaji.
Mratibu wa Mafunzo kituo cha Katavi akizungumzia mafunzo hayo.

Mkalawa amefafanua  kuwa, walimu na wathibiti ubora, watajifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya kisera yanayohusiana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023.

Amesema  mafunzo hayo yatajikita katika kutoa elimu inayohitajika kwa ajili ya kukabiliana na mahitaji ya sasa ya karne ya 21, ambayo inasisitiza ujuzi, ufundi na matumizi ya teknolojia.

Ameongeza  kuwa mbinu mpya za ufundishaji watakazofundishwa walimu zitasaidia kuongeza hamasa kwa wanafunzi kupenda kusoma  masomo hayo na kufanya vizuri kwenye mitihani.