Simba hii hata 'Nyuki' inaua tu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:38 AM Feb 03 2025
Wachezaji wa timu ya Simba
Picha: Mtandao
Wachezaji wa timu ya Simba

USHINDI wa mabao 3-0 iliyoupata Simba jana dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, umedhihirisha kuwa 'Nyuki' hao wa Tabora, si lolote kwa 'Mnyama' huyo hatari anapokuwa mawindoni kusaka alama tatu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Kwa ushindi huo umeifanya Simba kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Yanga juzi kukalia nafasi hiyo kwa muda kutokana na ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar na kufikisha pointi 42, mchezo ukichezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa Simba, yalikuwa ni mabao ya straika raia wa Cameroon, Leonel Ateba, aliyepachika mabao mawili na beki wa kulia, Shomari Kapombe, yaliyoifanya Simba kufikisha pointi 43, yakizima tambo za zaidi ya wiki moja za viongozi na mashabiki wa Tabora United.

Tabora United ilipata jeuri baada ya kuichapa Yanga mabao 3-1 na kisha kutoa kipigo cha 2-1 dhidi ya Azam FC kwenye mechi za mzunguko wa kwanza, matokeo yaliyoifanya kujiaminisha kwamba itaitandika pia Simba.

Kipigo hicho cha Tabora United kilifanana na kile cha mzunguko wa kwanza kilichotokea Agosti 17, mwaka jana, Uwanja wa KMC Complex, kwa mabao ya Che Fondoh, Malone, Velentino Mashaka na Awesu Awesu.

Kwa maana hiyo, Simba imezoa pointi zote sita na mabao sita msimu huu kutoka kwa 'Warina Asali' hao wa Tabora.

Pia Simba imerudia ilichokifanya msimu uliopita kwenye uwanja huo huo, Februari 6, mwaka jana, ilipoichakaza Tabora United mabao 4-0, yaliyowekwa wavuni na Pa Omar Jobe, Sadio Kanoute, Fredy Koublan na Che Malone.

Purukushani za Ateba kwenye lango la Tabora United zilianza dakika ya tatu tu ya mchezo, pale alipofanikiwa kuruka juu na kupiga kichwa mpira mrefu uliopigwa na Fabrice Ngoma, ukampita kipa, Jean Noel Amonone, lakini wakati ukielekea wavuni uliokolewa na beki Nelson Munganga.

Simba ilifanya shambulio lingine dakika nne baadaye, wakati Elie Mpanzu alipoambaa na mpira kwenye winga wa kushoto, akapiga krosi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wachezaji wenzake, lakini kipa Amonone, raia wa Gabon, aliyesajiliwa kipindi cha usajili wa dirisha dogo kutoka Arta Solar ya Djibouti, akawahi kuudaka.

Kichwa cha Kibu Denis pia kilidakwa na kipa huyo dakika ya nane, naye akiwekewa pasi ndefu ya juu na Ngoma.

Simba iliandika bao la kwanza dakika ya 12, mfungaji akiwa ni Ateba, kwa shuti kali la chinichini lililoonekana kama linakwenda nje, lakini mpira ukajaa ndani ya wavu.

Kabla ya kufunga alikuwa amepokea pasi kutoka kwa Mpanzu, akageuka na kuwahadaa mabeki wa Tabora United kabla ya kupachika mpira huo, kipa akiruka bila mafanikio.

Shambulio la kwanza la hatari kwa Tabora United kwa Simba lilifanywa dakika ya 30, wakati Offen Chikola, alipoupata mpira uliopigwa kichwa vibaya na Abdulrazack Hamza.

Akiwa pembeni kidogo, takriban yadi 30, aliachia shuti kali lililopaa juu kidogo ya lango la Simba.

Ateba alifunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 33, lililotokana na beki Pemba Kingu, kumuangusha Mpanzu ndani ya boksi.

Linakuwa ni bao la saba kwa Ateba kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu huu, akiwa ndiyo kwanza amesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea USM Alger ya Algeria.

Anakuwa kwenye nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji, akiwa na mabao sawa na mwenzake wa Simba, Jean Ahoua na Clement Mzize wa Yanga, huku kinara wao akiwa ni Elvis Rupia, Mkenya anayeichezea Singida Black Stars mwenye mabao manane.

Kapombe aliifungia Simba bao la tatu, likiwa ni la pili kwake msimu huu, akiunganisha pasi murua kutoka kwa Ateba.

Kazi nzuri iliyofanywa na Mpanzu ambaye jana alihusika katika mabao yote matatu, alimpenyezea Ateba, aliyeonekana kuwa kwenye jitihada za kutaka kupiga shuti na kufunga kiasi cha mabeki wote wa Tabora United kumkaba yeye, lakini alichofanya ni kuuachia kwa mfungaji aliyekuwa peke yake, akaukwamisha wavuni.

Timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa yaliyoufanya mchezo kuchangamka zaidi, huku kipa Moussa Camara akifanya kazi ya ziada dakika tano za mwisho, kwa kuchumpa na kukoa mashuti ya hatari kutoka kwa Nelson Munganga na Rajab Masinga. 

Ahoua pia alikaribia kufunga dakika za majeruhi kwa mpira wa mbali baada ya kipa kuonekana kusogea mbele ya lango.

Pamoja na kupoteza, Tabora United inabaki kwenye nafasi ya tano, ikiwa na pointi zake 25, kwa michezo 16 iliyocheza hadi sasa.