Watu wanaotaka kutumia dini kuvuruga amani wasivumiliwe

Nipashe
Published at 12:43 PM Jan 26 2025
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
Picha: Mtandao
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete

WIKI hii, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete alihudhuria kikao cha Kamati ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) na kuwaonya Watanzania kuacha kutumia mwamvuli wa dini kujenga chuki na mifarakano katika jamii hali inayochochea machafuko na uvunjifu wa amani.

Licha ya kutoa onyo hilo, aliwataka viongozi wa dini kusimama imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa  kisiwa cha  amani, utulivu, umoja na mshikamano. Pia aliwakumbusha kwamba amani na utulivu kamwe haviwezi kununuliwa dukani, hivyo ni lazima Watanzania waendelee kuimarisha undugu na mshikamano na kuepuka kubaguana kwa misingi yoyote ikiwamo ya kiimani, rangi na ukabila.

Kikwete ambaye ni mwasisi wa jumuiya hiyo, alikumbusha kuwa chachu ya kushauri kuanzishwa kwa taasisi hiyo enzi za serikali aliyoiongoza, ilisababishwa  na mgogoro wa kidini ulioibuka wa kuchinja, kati ya waumini wa Kiislam na Kikristo. Alisema  licha ya kuanzia eneo dogo la Katoro mkoani Geita, watu waliusambaza na kuuchochea kuwa wa kiimani na kusababisha machafuko, mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali.

Kutokana na kuwapo kwa mgogoro huo, Kikwete alisema hali ilikuwa mbaya kwa kuwa kila mmoja alichukua upande wake, ikabidi serikali ianze kuwadhibiti watu na vyombo vya habari vilivyoonekana kuuchochea. Pia alisema ilibidi serikali kuitisha mkutano uliowahusisha viongozi wa dini zote wakala na kunywa pamoja ili kila mmoja amzoee mwenzake na ndio ukawa mwanzo wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo. 

Rais huyo mstaafu alisema amani na utulivu ni tunu muhimu kwa taifa, hivyo viongozi wa dini hasa kupitia taasisi hiyo, wanapaswa kuendelea kusimamia amani, maadili na utulivu na kusaidia utatuzi wa migogoro mbalimbali ikiwamo ya wakulima na wafugaji. Pamoja na kutoa rai hiyo, Kikwete alionesha furaha yake kwamba hivi sasa migogoro hiyo imepungua tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015. 

Wahenga wanasema uzee ni dawa na ndivyo ilivyoonekana kwa Rais Mstaafu Kikwete alipozungumza kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha amani, upendo umoja na mshikamano ambavyo vimetamalaki nchini. 

Kwa maneno mengine, Mzee Kikwete amewakumbusha Watanzania kuwa amani si kitu cha kuchezea na pindi ikitoweka ni vigumu kuirejesha. Mfano wa hilo ni katika baadhi ya nchi ambazo wanaitafuta amani baada ya machafuko yaliyoacha maafa na majeraha miongoni mwa wananchi.

Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania wanaishi kwa amani na upendo bila kujali itikadi zao wala imani kwa kuwa ni wamoja na wanashirikiana katika masuala yote ya kijamii na katika shida na raha. Kwa hiyo mtu yeyote anayetangaza au kushabikia udini anakuwa si Mtanzania na nia yake si njema kwa jamii nzima na taifa kwa ujumla. 

Kama alivyosema Rais mstaafu, watu wanaochochea uvunjifu wa amani kwa kutumia mwamvuli wa dini wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa hawana nia njema na taifa la Tanzania. 

Kwa hali ilivyo sasa, dini si kigezo cha kuwagawa Watanzania kwa kuwa Waislamu na Wakristo wana historia ndefu iliyoota mizizi kwa kuwa wameoleana au hata katika baadhi ya koo, kuna watu wa imani zote hizo mbili. Hata wale wa madhehebu ya Ahmadia, Suni na Shia kwa Waislamu, wanashirikiana katika mambo yote na wanamwamini Allah ambaye ni Mungu. Jambo la kujiuliza wafarakane kwa sababu gani. 

Wakristo nao kama ilivyo kwa Waislamu wamegawanyika katika madhehebu mbalimbali na wote wanamwamini Mungu mmoja. Pia wanaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana  wa Mungu na ndiye atakayewahukumu wote siku ya kiama. Kama alivyosema Mzee Kikwete dini isitumike kuwagawa Watanzania na kusababisha uvunjifu wa amani.