BAADA ya Yanga kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kila mmoja anasema lake. Kila mmoja anatoa maoni yake ambayo yeye anadhani yamesababisha kushindwa kuingia hatua ya robo fainali, huku mashabiki wengi wakiitabiria mazuri.
Wengi walitarajia zaidi Yanga kushinda kuliko MC Alger kutoka sare kwenye mechi hiyo ya raundi ya sita hatua ya makundi, timu hizo zikiwa Kundi A.
Moja ya mambo niliyovutiwa nayo ni maneno ya Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, kudai Ligi ya Tanzania ni dhaifu na haizipi timu changamoto kiasi cha kuweza kupambana kwenye michezo ya kimataifa.
Akasema moja ya sababu ambayo timu yake ilikikosa kwenye mchezo dhidi ya MC Alger ni kuhimili kucheza na timu ngumu yenye wachezaji bora, wazoefu, waliotoka kwenye ligi bora, ambao kila wiki wanacheza mechi na timu ngumu.
"Tunapaswa kuwa wakweli kwamba ligi ya hapa Tanzania, ugumu unaokutana nao unapocheza dhidi ya timu nyingine za Tanzania si wa kiwango kikubwa sana. Ukiona ligi za Algeria, Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, ni wazi tunahitaji nguvu hiyo ya juu ili kushindana na kuweza kuzoea hali hiyo"
"Ukali wa Ligi ya Tanzania, ni mdogo sana ukilinganisha na nchi hizo, wao ligi yao ni ngumu na kila timu kali sana, tunahitaji ugumu kama wa ligi hizo ili tushindane," alisema kocha huyo.
Hakuna haja ya kufafanua sana alikuwa na maana gani. Ni kwamba urahisi wa kuzifunga timu za Tanzania, huwezi kuupata kwenye michezo ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho.
Hicho ndicho Yanga walichokutana nacho. MC Alger ilionekana waliweza kuikabili na kuhimili vishindo kwa sababu moja tu. Mechi kama hizi wanakutana nazo kwao wiki hadi wiki kwenye ligi yao.
Hapa Tanzania Yanga kupata aina hiyo ya mechi ni pale atakapocheza dhidi ya Simba, Azam, labda kwa sasa Tabora United.
Maneno aliyoyasema kocha wa Yanga yasipuuzwe kwa sababu yana ukweli kwa asilimia nyingi sana hususan kwa upande wa klabu hiyo.
Timu nyingi za Tanzania bado zina madhaifu makubwa, mabeki wanafanya makosa ya ajabu ya kujirudia ambayo yanasababisha timu kubwa zinashinda kirahisi.
Hapo bado, changanya na waamuzi wetu ambao wamekuwa na makosa mengi yanayoitwa ya kibinadamu, nao wanachangia kuifanya ligi kuonekana dhaifu na kutowapa wawakilishi wetu upinzani.
Kama vile haitoshi, wadau wa soka wamekuwa wakipiga kelele juu ya mdhamini mmoja kudhamini timu zaidi ya tano kwenye ligi, kitu ambacho kinaondoa kile kinachoitwa 'fair play' kwenye soka.
Vyovyote itakavyokuwa, hata kama klabu zinahitaji pesa, lakini mdhamini wa kampuni ambayo mpaka inalipa mishahara ya wachezaji wa klabu moja, ikifanya kila kitu kama vile imenunua hisa, kwenda tena kudhamini klabu zingine, huwezi kutegemea upinzani mkubwa kwenye baadhi ya michezo ya ligi kwa timu hizo zinapokutana.
Hata hivyo, hapa kuna cha kujiuliza. Kama ni hivyo ni kwa nini Simba imekuwa ikifanya vema kwenye michezo ya kimataifa kwa misimu kadhaa sasa nchini wakati nayo ipo kwenye ligi hiyo hiyo?
Je, kuwapo kwa ahadi za pesa zinazoahidiwa kila timu inayocheza na Simba ndiyo kunaifanya timu hiyo kuwa imara? Ni jambo la kujiuliza.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na wadau wote wa soka, wanapaswa kuliangalia hili, kwani huyu si kocha wa kwanza kuongea maneno haya.
Nakumbuka hata kocha wa zamani wa Yanga, aliwahi kubainisha hili. Hawa makocha hawaongei kwa bahati mbaya. Kuna kitu wamekiona. Bahati nzuri kwa sasa nchi yetu ina wachezaji wengi bora kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakimiminika kucheza soka la kulipwa. Kwa maana hiyo ikiwamo tu dhamira ya dhati, Ligi ya Tanzania inaweza kuwa bora hata msimu huu.
Tatizo ni kwamba soka la Tanzania limekuwa na siasa zaidi kuliko uhalisia ya mchezo wenyewe. Tukiacha siasa na kuacha soka lichezwe kila mechi itakuwa ngumu. Kila wiki timu zetu zitakutana na michezo migumu. Linaweza kabisa kutusaidia huko mbele kwenye michezo ya kimataifa kama Ramovic anavyotaka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED