FEBRUARI 10 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kifafa Duniani ambayo huadhimishwa kwa lengo la kutoa takwimu kuhusu madhara ya ugonjwa huo na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa katika kupambana na tatizo hilo.
Ugonjwa wa kifafa husababishwa na mambo mbalimbali yakiwamo ulaji nyama ya nguruwe isiyoiva ipasavyo, ajali, uzazi pingamizi na mbung’o katika baadhi ya maeneo hasa ya kitropiki ambayo huchangia kuzaliana kwa wadudu hao.
Takwimu zinaonesha kuwa kifafa ni ugonjwa wa kudumu wa ubongo unaoathiri takribani watu milioni 60 na inakadiriwa kwamba watu 34 hadi 76 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaongezeka kila mwaka, ukiwa ni wastani wa uwiano wa asilimia 0.5 hadi moja.
Nchini Tanzania, athari ya jumla ya muda wote ni asilimia mbili huku Afrika ikiwa na idadi kubwa ya walioathirika ambao ni kati ya watu 20 na 58 kwa kila watu 1,000. Utafiti uliopita na wa sasa umeonesha kuwa takribani watu milioni moja wanaishi na kifafa nchini.
Aidha Mahenge katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na Hydom, Mbulu mkoani Manyara yanatajwa kuwa ni maeneo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa. Ulanga ina wagonjwa wengi kutokana na ongezeko la mazalia ya mbung’o huku Hydom ikitajwa kuwa inaongoza kwa ulaji wa nyama ya nguruwe, ikiwamo ile isiyoiva kwa kiwango kinachotakiwa.
Taarifa zinabanisha kwamba kitimoto (nyama ya nguruwe) isipoiva ipasavyo, husababisha minyoo ambayo husafiri hadi kichwani na kuziba damu kupita ipasavyo. Kutokana na hali hiyo, mlaji wa nyama hiyo, hasa ambayo haijaandaliwa kwa ufasaha na kuiva kwa kiwango kinachotakiwa, mlaji anaweza kukumbwa na ugonjwa huo.
Takriban miaka 30 sasa, nyama ya nguruwe, maarufu kama kitimoto,imejipatia umaarufu mkubwa nchini na kupendwa na watu wengi. Watu wengi wamekuwa wakifika kwenye sehemu za starehe kama vile baa ambako nyama hiyo imekuwa ikiuzwa kwa wingi kama asusa au mlo kamili sambamba na ugali au ndizi.
Pia zimeanzishwa bucha mbalimbali za nyama hiyo kila kona hasa kwenye miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro na Iringa. Jambo la kujiuliza ni je, kuwapo kwa biashara hiyo katika maeneo mbalimbali, wahusika wana uelewa kuhakikisha nyama hiyo inaiva ipasavyo na kutoathiri watu kukumbwa na maradhi mbalimbali, ikiwamo kifafa?
Kwa ujumla, biashara ya nyama ya nguruwe, kitimoto kama inavyojulikana, inashika chati ya juu katika ulaji kwa sasa lakini kutokana na taarifa kwamba ni moja ya vyanzo vya maradhi ya kifafa, tahadhari inapaswa kuchukuliwa ili isisababishe madhara kwa binadamu hasa watumiaji.
Kama Chama cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania (TEA) kilivyoainisha tatizo hilo, ni vyema elimu ikatolewa kuanzia muuzaji wa nyama hadi mtumiaji ili kuhakikisha uandaaji wa kitoweo hicho unafanyika katika viwango vinavyotakiwa ili kutoleta madhara ya kiafya.
Kutokana na nyama hiyo kupendwa na watu wengi, hivyo imechangia kuwapo kwa ajira kuanzia kwa wafugaji, wachinjaji na wauzaji. Kwa mantiki hiyo, suala hapa si kukataza watu kutumia bali kuhimiza iandaliwe kwa viwango stahiki ili isisababishe maradhi yakiwamo ya kifafa.
Suala la afya bora linaanza na mtu mmoja mmoja kisha jamii na taifa kwa ujumla ikiwamo kuchukua tahadhari kuhusu matokeo ya jambo fulani. Kwa hiyo katika kujikinga na kifafa kupitia ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo haijaiva kama inavyotakiwa, ni vyema kila mtu achukue hatua kujilinda na tatizo hilo
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED