KATIKA Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika kuanzia Desemba 21, mwaka huu huko Morocco, Tanzania (Taifa Stars), imepangwa katika Kundi C ikiwa pamoja na Nigeria, Uganda na Tunisia.
Baada ya droo hiyo kufanyika, kumezuka mijadala mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wadau na mashabiki wa soka juu ya ugumu wa kundi ambalo Taifa Stars iko.
Wengi hawasemi ni kundi la kifo, ila ni kundi gumu ambalo hawana uhakika kama Stars inaweza kutoboa na kusonga mbele hatua inayofuata.
Sababu kubwa ni timu wapinzani ambao wamepangwa kundi moja.
Nigeria ni moja kati ya majina makubwa si barani Afrika tu, bali dunia nzima linapokuja suala la mpira wa miguu.
Tunisia nayo ni hivyo hivyo, ni moja kati ya timu kubwa ya 'kutisha' linapokuja suala la soka Afrika na duniani pia.
Uganda siyo timu ngumu au yenye jina sana kwenye soka Afrika, lakini ni moja kati ya timu inayoipa ugumu na changamoto kubwa Tanzania zinapokutana, iwe katika timu za wakubwa, wanawake mpaka kwa vijana wa umri wote.
Kwa sasa mpinzani mkubwa wa soka la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa Tanzania ni Uganda.
Na hata matokeo yake huku hayajulikani yatakuwaje zinapocheza.
Oktoba tu mwaka jana, timu za Tanzania na Uganda zilikutana katika mechi za kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Afrika chini ya miaka 20. Katika mchezo wa nusu fainali, lakini kwenye mechi ya AFCON chini ya miaka 17 iliyochezwa hapa nchini, Uganda ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa fainali. Hii inaonyesha upinzani uliopo.
Hakuna anayepinga Kundi C ni gumu, lakini kinachotakiwa ni kujipanga na si kuogopa.
Kwa miaka ya hivi karibuni tumeanza kuona baadhi ya nchi ambazo zamani zilikuwa chini kisoka na zilikuwa zikipigwa mabao mengi, zikianza kuwa tishio kwa yale mataifa makubwa ambayo yalionekana hatari.
Mfano timu kama Cape Verde, Comoro, Equatorial Guinea, Botswana, hazikuwa juu kisoka na hata zinapopangwa na timu iwe klabu au timu za taifa, moja kwa moja timu zingine zinaona zimepata mchekea, lakini siyo sasa.
Kwa sasa ukipangwa nazo jiandae kisawaswa, si tena wale wa miaka ile ambao walitambulika kama vibonde.
Hapa ukiondoa Cape Verde tu ambayo haijafuzu AFCON, zote ninazokutajia zimefuzu, kitu ambacho ilikuwa nadra sana kukikuta miaka ya 1970, 1980, 1990, hadi miaka ya 2000.
Hivi ninavyoandika, Comoro iko Kundi A, huyu huyu kibonde wa miaka ya 1980 hadi 1990.
Ilikuwa ni ajabu kukuta timu hiyo ikishinda hata mchezo mmoja tu. Equatorial Guinea ipo Kundi E, Botswana nayo imetupwa Kundi D.
Na tusishangae katika AFCON 2025, nchi hizo, timu zisizotegemewa ndiyo zinaweza kushangaza wengi na kufuzu hatua inazofuata.
Soka kwa sasa dunia limebadilika kabisa, ni kujipanga, mfumo, mbinu na nidhamu ya wachezaji ndivyo vinavyoamua uwanjani timu gani ishinde.
Zile zama za kutegemea vipaji vya machezaji mmoja mmoja kuamua mechi kama kina Nwanko Kanu, Austin Jay Jay Okocha, Maradona, Pele, zimepitwa na wakati na inaonekana kwa sasa aina ile ya wachezaji kama haipo basi imepungua sana.
Watanzania tusitishwe na majina ya nchi kubwa za mpira kwa wakati huo. Kwa sasa soka la nchi hii limepiga hatua sana na wala si ajabu Stars ikavuka kwenda raundi ya pili.
Kinachotakiwa ni kufanyika kwa uteuzi mzuri wa wachezaji ambao wana viwango bora kwa wakati husika, pamoja na maandalizi ya kina. Hakuna kinachoshindikana kuondoka na mmoja kwenda hatua inayofuata au kufika robo fainali, haidhuru kuwaacha wote wawili tukaondoka na Uganda.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED