Watumishi waliogeuka kuwa mawakala wa wagombea waonywa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:50 PM Jan 31 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Picha:Shaban Njia
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameonya vikali baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Ushetu waliogeuka kuwa mawakala wa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge, akisema ataagiza wafukuzwe kazi ili kuepusha kuchanganya siasa na kazi za serikali.

Macha alitoa onyo hilo jana katika Kata ya Kisuke alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hali ya uzalishaji wa zao la pamba na kusikiliza changamoto za wakulima, hususan upatikanaji wa viuatilifu na mabomba ya kupulizia dawa za kuua wadudu shambani.

Alibainisha kuwa baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wameacha majukumu yao na badala yake wanashiriki katika siasa kwa kuwatafutia kura wagombea wa nafasi mbalimbali, jambo ambalo halikubaliki. Alisisitiza kuwa hatasita kuiwasilisha orodha ya watumishi hao kwa Mkuu wa Wilaya ili hatua zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.

“Nina orodha ya baadhi yao ambao badala ya kufanya kazi walizotumwa na serikali, wamegeuka kuwa wanasiasa. Nitaikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ili ichunguzwe, na wale watakaobainika tutaagiza mamlaka husika ziwafute kazi ili waendelee na siasa zao huko,” alisema Macha.

Aliwataka watumishi hao kuwaacha madiwani na wabunge wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria badala ya kuwahimiza kuwapitisha wagombea kabla ya muda sahihi. Alisisitiza kuwa vyama vya siasa vina taratibu zao za uteuzi pindi muda wa uchaguzi utakapowadia.

Aidha, aliwasihi watendaji wa vijiji na kata, maafisa elimu na maafisa kilimo kufanya kazi zao kwa uadilifu na kuepuka kujihusisha na masuala ya kisiasa ambayo yanaweza kuhatarisha ajira zao. “Wanasiasa huwa na kawaida ya kugombana na baadaye kupatana, lakini wewe kama mtumishi wa umma unaweza kupoteza ajira yako bure,” alionya.

Macha aliwataka watumishi wanaotamani kuingia kwenye siasa kusubiri muda sahihi na kujitokeza wazi pindi mchakato wa uchaguzi utakapofika badala ya kufanya kampeni kisiri. Alisisitiza kuwa wakati huu ni wa kuwahudumia wananchi na kuhakikisha uzalishaji wa pamba unaongezeka ili kufikia viwango vya mazao mengine ya biashara kama tumbaku.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, aliwataka watendaji kushirikiana naye katika kuongeza uzalishaji wa pamba kwa kuwahamasisha wakulima kutumia mbinu za kisasa. Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha mkulima mmoja anavuna kilo 1,200 kwa ekari badala ya kilo 300 wanazopata sasa.

Aliongeza kuwa Kata ya Kisuke ina mradi wa kuwafundisha vijana kilimo chenye tija, ambapo zaidi ya ekari 900 zimetengwa na matrekta mawili yametolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa ajili ya kufanikisha mradi huo.

Ofisa Kilimo wa Kisuke, Soud Njalamoto, alisema kuwa kuna zaidi ya wakulima 208 wanaojishughulisha na kilimo cha pamba katika eneo hilo. Alisisitiza kuwa wamepatiwa elimu juu ya mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya viuatilifu, na udhibiti wa wadudu waharibifu ili kufanikisha lengo la uzalishaji lililowekwa na serikali.

Mkoa wa Shinyanga unatarajia kuona ongezeko kubwa la uzalishaji wa pamba huku serikali ikiendelea kuimarisha mikakati ya kuinua sekta ya kilimo kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa taifa kwa ujumla.