DAR- kuzindua biashara saa 24 Februari 22 mwaka huu

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 02:38 PM Jan 31 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila.
Picha: Iman Nathaniel
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila, ametangaza rasmi kuwa jiji la Dar es Salaam litaanza shughuli za biashara saa 24, ambapo uzinduzi rasmi utafanyika Februari 22, 2025.

 Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, Januari 30, 2025, RC Chalamila amesema maandalizi yanaendelea vizuri, ambapo taa za barabarani na kamera za usalama zinaendelea kufungwa ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa shughuli za biashara katika jiji hilo.

RC Chalamila alisisitiza kuwa jiji la Dar es Salaam ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa, na kwa hivyo, mkoa utazindua rasmi mpango wa kufungua biashara saa 24 ili kuwezesha uchumi na kuongeza ajira. Aliongeza kuwa tayari wanaendelea na maandalizi ya kutosha ya usalama, kwa kuzingatia uwekaji wa taa na kamera.

Akizungumzia Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam, RC Chalamila aliwashukuru wananchi wa mkoa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha amani, utulivu, na usafi wa mazingira. Aliwahimiza viongozi wa wilaya zote za mkoa kuhakikisha kuwa suala la usafi linaendelea kushughulikiwa ili jiji liendelee kuwa kivutio kwa wawekezaji na wageni.

Pia, alizungumzia mpango wa serikali wa kuimarisha usafiri jijini, akieleza kuwa utaratibu wa usafiri wa treni na majini unatarajiwa kuanza kutumika ili kuboresha usafiri wa ndani ya jiji hilo.

Kuhusu ujenzi wa Soko la Kariakoo, RC Chalamila alifahamisha kuwa zaidi ya bilioni 28 zimetelewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo na kwamba ujenzi umefikia asilimia 97. Aliongeza kuwa kwa sasa bodaboda na bajaji hazijazuiliwa kuingia katikati ya jiji, baada ya zuio lililowekwa kwa ajili ya ugeni wa marais wa Afrika.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Soko la Kariakoo, Hawa Ghasia, alieleza kuwa kuanzia Januari 31, 2025, watakianza kuweka majina ya wafanyabiashara waliokuwa wakiendesha biashara katika soko hilo kabla halijaungua ili wasajiliwe. Baada ya hiyo, watasajili wafanyabiashara wapya na pia wafanyabiashara waliokuwa na madeni watahitajika kulipa madeni yao.

Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kuwa na mageuzi makubwa katika sekta ya biashara, usafiri, na miundombinu, na hatua hizi zinaonesha kuendelea kwa juhudi za kuboresha mazingira ya kibiashara na ustawi wa wananchi.

5