Jengo la Kariakoo laibua yaliyofichwa

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:28 AM Jan 31 2025
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

KUPOROMOKA kwa jengo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam kumeibua 'madudu' mengi yaliyokuwa yamefichika, ukiwamo udanganyifu kwenye maghala ya kuhifadhi mizigo na chanzo cha kuungua kwa Soko Kuu la Kariakoo.

Vilevile, uchunguzi wa tukio hilo umebaini mambo mengine ya ziada yakijumuisha ongezeko la wageni wanaofanya kazi za wazawa, shehena za magendo katika maghala ya Kariakoo na msongamano wa machinga kwenye barabara, hata kulazimu serikali kutangaza mpango wa kujenga Kariakoo mpya kwenye eneo la Jangwani.

Rais Samia Suluhu Hassan alitaja 'madudu' hayo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam alipokutana na kula chakula cha mchana na watu walioshiriki uokoaji kwenye jengo la ghorofa lililoporomoka Kariakoo mnamo Novemba 16, 2024.

Alisema wingi wa mizigo kwenye jengo lililoporomoka ulichangia ajali hiyo kwa kuwa lilikuwa na uwezo wa kubeba tani 250, lakini lilikutwa na tani 850 za mzigo.

Rais Samia alisema taarifa ya awali kutoka kamati iliyochunguza jengo lililoporomoka, imebaini pia udanganyifu kwenye maghala ya kuhifadhi mizigo.

"Tumepata somo la jinsi biashara inavyoendeshwa pale Kariakoo. Tumeelezwa hapa kwamba jengo lile lilikuwa na uwezo wa kuchukua tani 250 za mzigo, lakini tani zilizokuwepo pale ni 850. Kwa hiyo kwa vyovyote vile lisingeweza kubeba. Hili ni jengo moja, nina hakika majengo mengi yaliyoko Kariakoo yako katika mfumo huu.

"Ambalo mimi nililiona kwa harakaharaka na pengine ndilo kwa wakati ule lilileta mzozo wa wafanyabiashara wa Kariakoo, ni mali iliyofichwa mle ndani na pengine bila kulipiwa kodi.

"Sasa jengo lile limetufunulia tu mambo mengi. Sidhani kama tani zile 800 zililipiwa kodi na ndiyo maana TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ilipeleka watu kuangalia maghala eneo la Kariakoo. Hili ni somo lingine ambalo tumelipata," alisema.

Rais aliielekeza TRA kuweka mazingira sawa ya ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wote, ili kuweka mazingira ya haki ya ufanyaji biashara.

SOKO JANGWANI

Kukiwa na maombi ya uongozi wa Klabu ya Yanga kujenga uwanja wa kisasa Jangwani, Rais Samia alisema serikali inakusudia kujenga soko kubwa na la kisasa kwenye eneo hilo. Litatumiwa na machinga, hivyo kupokea kilio cha wafanyabiashara kuwa barabara nyingi za Kariakoo zimevamiwa na machinga.

Alisema serikali inataka biashara zifanyike kwa saa 24 Kariakoo, hivyo ulinzi na miundombinu ya barabara inapaswa kuwa wazi na kupitika wakati wote.

"Wafanyabiashara ndogo wameziba njia na kujenga maduka barabarani. Tume wameliona hili, niwaombe tutakapokuja kutekeleza mapendekezo ya tume, mshirikiane nasi. Dar es Salaam tuna mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu (DMDP), ambao kati ya fedha zake, tumejipanga kujenga soko lingine kubwa na zuri kama la Kariakoo, maeneo ya Jangwani. 

"Kwa hiyo, ni maoni yetu kwamba baadhi ya wafanyabiashara, wanangu machinga tutawahamisha tuwapeleke kwenye soko lile la Jangwani, wakafanye biashara zao kule kwa nafasi na kwa vizuri," alisema.

MOTO KARIAKOO

Rais Samia pia alitaja chanzo cha kuungua Soko Kuu la Kariakoo Julai 10, 2021 ni njama zilizolenga kupoteza ushahidi wa kilichokuwa kinaendelea sokoni huko.

"Nilikuja Kariakoo na baada ya kuondoka tu, siku iliyofuata mkalitia moto. Baada ya kuzisema changamoto za uongozi uliokuwapo na mambo yaliyokuwa yanafanyika katika soko na kuvitaka vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi ndani ya soko, ili kupoteza ushahidi mkalichoma moto, lakini kwa ujasiri nikaamua kulijenga tena," alisema.

Alisema serikali imejifunza mambo manne baada ya kuporomoka kwa jengo, ikiwa ni pamoja na utanuzi wa majengo Kariakoo unaofanywa kwa msingi wa awali badala ya kujenga upya kulingana na ukubwa wa jengo.

"Tunarefusha juu, tunachimba chini, lakini kwa msingi uleule wa mwanzo. Hii ni hatari," alisema Rais na kusisitiza kuwa kuepusha hasara ya mali na maisha ya wananchi, serikali itaimarisha usimamizi wakati wote wa ujenzi.

MPANGO UJAO 

Alisema katika mipango ya baadaye, katika kukabiliana na maafa, serikali itanunua vifaa na rasilimali kusaidia uokoaji ili kukabiliana na maafa kwa ufanisi. Alisema vifaa vingi vya uokoaji vilivyotumika Kariakoo, vilikuwa vya sekta binafsi ambavyo serikali ilipaswa kuwa navyo.

Alisema serikali pia itaimarisha mifumo ya maafa na kuzijengea uwezo timu za usimamizi wa maafa za mikoa na wilaya, ili ziwe tayari kuyakabili yanapotokea.

"Tutahakikisha viwango vya ubora vya ujenzi vinazingatiwa ipasavyo na taratibu za ukaguzi wa majengo zinaimarishwa. Sheria za ujenzi zinafuatwa na rasilimali za kiufundi zinapatikana kwa ajili ya kusimamia sekta hiyo muhimu," alisema Rais Samia.

WAGENI MACHINGA

Rais Samia pia alimwelekeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo, kuhakikisha biashara za wazawa hazifanywi na wageni.

"Kuna kipindi nilirushiwa 'clip' mgeni anapigana na mwenyeji Kariakoo, nikasema 'huyu ni machinga wameshindwana kwenye shughuli zao...' haiwezekani mgeni akawe machinga, vijana wetu watafanya biashara gani? Waziri wa Biashara simamia hili," aliagiza.

SABABU ZA KUKOPA

Mkuu wa Nchi pia alitoa sababu za serikali yake kuendelea kukopa, akisisitiza ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, shule na hospitali.

"Asiyejua anasimama anasema 'hii serikali kazi kukopa tu', kwani tunakopa kwenda kununua sare za harusi? Tunakopa kujenga reli, barabara, shule, huduma za afya, kufanya Dar es Salaam na Dodoma kuwa miji mikubwa inayoheshimika, tunakopa kukuza hadhi ya nchi yetu. Hakuna anayependa kukopa, tunakopa kwa sababu," alisema.

Rais Samia aliwataka wafanyabiashara kulipa kodi stahiki ili nchi ipunguze kukopa na kuomba misaada, akisema "kila anayefanyabiashara akichangia kidogo kidogo, kile kiwango cha kukopa kitapungua. Tutaendesha mambo mengi, kwa fedha tunayokusanya ndani. Niwaombe sana, tukashirikiane kwenye hilo.

"Kodi hizi ni mnayaona yanayotokea ndani ya nchi. Tusipolipa kodi na kuacha wachache walipe na kubeba wengi wasiolipa kodi, hii ni hasara kubwa kwa taifa," alisema.

Rais alisema hivi sasa TRA inakusanya wastani wa Sh. trilioni tatu kwa mwezi na kwamba lengo ni kukusanya Sh. trilioni nne kwa mwezi miaka michache ijayo na ikiwezekana mwakani, Hilo litawezekana kama mzunguko wa ufanyaji biashara na uwekezaji utaongezeka.

Hata hivyo, alisema wafanyabiashara wengi wa kati na wadogo wanakimbia kulipa kodi.

Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema kwenye uokoaji Kariakoo, ziliokolewa fedha na marobota ya nguo yenye uzito wa tani 850.

Alisema ziliokotwa Sh. milioni 112.8, Dola za Marekani 48,490, fedha za China Yuan 631 na Sh. 6,920 za Kenya. Fedha hizo zote zimeendelea kurejeshwa kwa wamiliki waliotambuliwa.

Alisema kamati ya kuchunguza jengo lililoporomoka pamoja na majengo mengine, tayari imekamilisha kazi na kuwasilisha kwake na kwamba iko tayari kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Rais.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi, aliwasilisha maombi mawili kwa Rais Samia; usawa wa kikodi uwekwe kwa wafanyabiashara na kuwaondoa machinga barabarani ili biashara zifanyike kwa wepesi Kariakoo.

Katika tukio hilo la Novemba 16 mwaka jana, watu 31 walipoteza maisha na wengine 71 waokolewa na kutibiwa.

Manusura wa tukio hilo la Kariakoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Jengo Lililoporomoka, Martilda Zela, alisema wafanyabiashara walipoteza mitaji. Hadi sasa hawajarejea kwenye hali yao ya awali.