Serikali za Afrika Kusini na Rwanda zimeingia katika mzozo kutokana na vita vinavyoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya wanajeshi 13 wa Afrika Kusini kuuawa katika uwanja wa mapambano.
Kufuatia vifo hivyo, serikali ya Afrika Kusini imetoa taarifa kupitia mtandao wake wa kijamii wa X (Twitter), ikitoa salamu za pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuishutumu Rwanda kwa kushirikiana na waasi wa M23 katika mashambulizi hayo.
Baada ya tamko hilo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alikanusha tuhuma hizo, akizitaja kuwa za uongo na kinyume na mazungumzo aliyokuwa nayo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Kagame alidai kuwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) si kikundi cha waasi bali ni jeshi rasmi la Rwanda, akidai kuwa misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC) inalenga kushambulia wananchi wa DRC na kuivamia Rwanda kijeshi.
"Wapendwa Wananchi wa Afrika Kusini, kutokana na kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC, tumepoteza wanajeshi wetu 13 shujaa waliokuwa wakipigania amani.
Mapigano haya yamechochewa na waasi wa M23 kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) dhidi ya Vikosi vya FARDC na walinda amani wa Misheni ya SADC (SAMIDRC).
Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Afrika Kusini, tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na tunawaenzi kwa ujasiri wao. Msaada wote muhimu unapatikana kwa familia zilizoathirika, huku taratibu za kuwarejesha nyumbani waliofariki zikiendelea.
Mashambulizi haya yameathiri pia wanajeshi kutoka Malawi, Tanzania, na wanachama wa MONUSCO. Hali katika Goma na Sake bado ni tete na isiyotabirika, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha vikosi vya SAMIDRC vinapokea msaada wa kutosha.
Uwepo wa wanajeshi wetu mashariki mwa DRC haupaswi kutafsiriwa kama tangazo la vita dhidi ya taifa lolote, bali ni juhudi za kuleta amani chini ya Umoja wa Mataifa na SADC. Tunasisitiza pande zote kushiriki juhudi za kidiplomasia ili kupata suluhisho la kudumu."
Rais Kagame alijibu madai ya Afrika Kusini kwa kusema:
"Nimefanya mazungumzo na Rais Ramaphosa kuhusu hali mashariki mwa DRC, lakini taarifa zinazotolewa na maafisa wa Afrika Kusini ni potofu na za upotoshaji.
Mzozo kati ya Afrika Kusini na Rwanda unaendelea kuwa na mvutano mkubwa, huku pande zote zikitupiana lawama kuhusu mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC. Ingawa juhudi za kidiplomasia zinahitajika, mvutano huu unaonyesha ugumu wa kuleta amani katika eneo hilo lenye migogoro ya muda mrefu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED