VIONGOZI wa dini, wametakiwa kutumia majukwaa ya dini na nyumba za ibada, kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema hayo leo Januari 30, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran Tukufu.
Amewataka viongozi hao kutoa mafunzo na maadili mema, hasa kwa vijana kwa kuwa elimu ya dini wanayoitoa inajenga maadili na kudumisha amani ndani ya nchi.
"Kwa kupitia mafunzo yenu ya dini mnayoyatoa, kwa kupitia watoto wetu, inafanya kuwe na jamii yenye hofu ya Mungu na hiyo ni chachu ya kudumisha amani,” amesema.
Aidha, amesema serikali inaziunga mkono taasisi za dini zote, kwa kuwa inasaidia sana kudumisha uhuru na umoja uliopo na nchi jirani na zingine kuvutiwa na amani iliyopo nchini.
Mwenyekiti wa tuzo, Shekhe Othuman Kaporo, ameviambia vyombo vya habari kuwa, kilele cha tuzo hizo kitakuwa Februari 23, 2025 zikifanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kaporo amesema mashindano hayo kwa mwaka huu, yatakutanisha vijana kutoka mabara matano ya duniani, ikiwamo Afrika, Australia, Asia, Ulaya na nchi 25 zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo.
Pia, amebainisha lengo la mashindano hayo ni kuboresha malezi na maadili, kuleta chachu ya maadili mema katika jamii na kupenda kuhifadhi maneno ya Mwenyezi Mungu.
Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Walidi, amesema kupitia mashindano hayo, ni kumuunga mkono Rais Samia, kudumisha 4R na kudumisha amani nchini.
Amesema wazazi wajikite kuwapeleka watoto kupata elimu ya dini, ili kuepusha mmomonyoko wa maadili katika jamii. Kauli mbiu ya mashindano hayo ni KURUAN NI AMANI.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED