Meya Arusha azindua mitambo ya kisasa ukarabati wa barabara

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 07:28 PM Jan 30 2025
Meya Arusha azindua mitambo ya kisasa ukarabati wa barabara.
Picha:Mpigapicha Wetu
Meya Arusha azindua mitambo ya kisasa ukarabati wa barabara.

Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iraqhe, leo amezindua rasmi mtambo mpya wa kutengeneza barabara pamoja na malori mawili mapya, yaliyotolewa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji hilo, zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Arusha, Meya Iraqhe amewataka madiwani kushirikiana na wananchi katika kuainisha barabara zenye uhitaji wa ukarabati ili mitambo hiyo iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

"Vifaa hivi vimenunuliwa kwa fedha za wananchi kupitia mapato ya ndani ya Jiji. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunavitunza ili viweze kudumu kwa zaidi ya miaka kumi," alisema Iraqhe.

Mtambo huo pamoja na malori mapya yameanza kazi mara moja katika Kata ya Olorien, Murieti, Moshono na Olasiti, kabla ya kuendelea kwenye kata zingine.

Barabara za mitaa kunufaika na ukarabati

Kwa mujibu wa Iraqhe, mitambo hii itajikita katika kutengeneza barabara za mitaa zisizofikia vigezo vya kutengenezwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ambao wanakarabati barabara zenye upana wa mita 12 na zaidi.

"Kwa kuwa barabara nyingi za mitaa zina upana wa chini ya mita 12, mitambo hii ya Jiji la Arusha itahakikisha zinawekwa katika hali nzuri. Ukarabati huu unaanza mara moja," ameongeza Meya Iraqhe.

Viongozi watambua juhudi za maendeleo

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, John Kayombo, amesema kuwa mitambo hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya barabara mbovu katika jiji hilo na kuwezesha wananchi kufanikisha shughuli zao kwa urahisi.

"Sasa hata mitaa ambayo awali Meya ulikuwa hupiti, utaweza kupita kwa sababu mitambo hii itakarabati barabara zote," amesema Kayombo.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Ujenzi wa Jiji la Arusha, Jacob Mwakyambiki, alieleza kuwa lengo la ununuzi wa mtambo huo ni kukarabati barabara zote za kata 25 na mitaa yake, ili kuboresha miundombinu ya usafirishaji ndani ya Jiji la Arusha.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kuahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.

"Natoa ahadi ya kushirikiana na watumishi wa umma wenzangu kulinda imani ya Arusha na kuhakikisha tunawatumikia wananchi kwa uadilifu," amesema Rombo.

3

CCM wapongeza juhudi za maendeleo

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk. Wilfred Soilel, amepongeza juhudi za Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kununua mitambo hiyo, akisema kuwa uamuzi huo utasaidia kupunguza kero ya barabara mbovu.

"Barabara nyingi za jiji letu zina upana wa mita 7 au 8, hivyo TARURA wasingeweza kuzikarabati kwa kuwa wao wanashughulika na barabara za kuanzia mita 12. Bila uamuzi huu, barabara nyingi zingebaki katika hali mbaya," alisema Dkt. Soilel.

Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa Jiji kuhakikisha kuwa mitambo hiyo inatunzwa vizuri na kuepuka ubadhirifu wa vifaa vyao vya kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Khamana Simba, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Morogoro, alitumia hafla hiyo kuwaaga wananchi wa Arusha, akisema kuwa ataendelea kutumikia taifa kwa bidii katika nafasi yake mpya.

"Tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa hapa Arusha, sasa nakwenda kuwatumikia wananchi wa Ulanga," alisema Simba.

Uzinduzi wa mitambo hii unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya barabara za mitaa jijini Arusha, na hivyo kuinua hali ya uchumi kwa wananchi wa jiji hilo.