Tshisekedi aionya M23, atangaza mashambulizi makali kuwaondosha

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:18 PM Jan 30 2025
news
Picha:Mtandao
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Félix Tshisekedi.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Félix Tshisekedi amekionya kikundi cha waasi wa M23 akitangaza matumizi ya nguvu kutoka jeshi la DRC dhidi ya kundi hilo alilolitaja kuungwa mkono na Rwanda.

Tshisekedi amesema hayo usiku wa jana Januari, 29 na kueleza kuwa vikosi vya jeshi lake vinaendelea kupiga hatua kali za kijeshi huku wapiganaji wa M23 wakizidi kusonga mbele mashariki mwa nchi hiyo.

Félix Tshisekedi akihutubia Taifa hilo kwa njia ya televisheni kwa mara ya kwanza tangu M23 iingie jijini, Tshisekedi alisema mashambulizi makali na yaliyoratibiwa dhidi ya magaidi hao na wafadhili wao yanaendelea.

Aidha alilaani kutochukua hatua kwa jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na kile alichokieleza kuwa kuzorota kwa hali ya usalama kusiko na kifani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa mara ya pili ndani ya siku tatu siku ya Jumanne kujadili mzozo unaozidi kuongezeka mashariki mwa DRC, likitoa wito kwa M23 kusitisha mashambulizi yake.

Akihutubia Baraza hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner, aliomba hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Alisema hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ni pamoja na kuondoa waasi hao katika ardhi ya Kongo na kuweka vikwazo dhidi ya jeshi la ulinzi la Rwanda.

Jana jumatano Januari 29, Rais Tshisekedi hakuhudhuria kwenye mkutano wa dharura wa kilele wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioandaliwa na Kenya, ambao ulihudhuriwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Hatahivyo taarifa baada ya mkutano huo, wakuu wa nchi wa kanda hiyo walitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita hiyo na kutaka suluhisho la amani la mzozo huo.

Pia waliitaka Kinshasa kushiriki moja kwa moja na washikadau wote, ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza M23 na makundi mengine yenye silaha ambayo yana malalamiko.

Viongozi wa Afrika Mashariki walisema wanapanga kufanya mkutano wa pamoja kuhusu mgogoro huo na viongozi kutoka kusini mwa Afrika katika siku zijazo.

Angola, ambayo ilisuluhisha jaribio lililoshindwa la mazungumzo mwezi uliopita kabla ya M23 kuanza mashambulizi yake, ilitoa wito kwa viongozi wa Kongo na Rwanda kukutana haraka mjini Luanda.

Ofisi ya Rais wa Angola ilisema Rais wa DRC yuko katika mji mkuu wa Angola siku ya Jumatano kwa mazungumzo kuhusu hatua zinazofuata.

Waasi wa M23 wameteka eneo lenye utajiri wa madini katika wiki za hivi karibuni, ukiwemo mji mkuu wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Kinshasa, Umoja wa Mataifa, Marekani, na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi yalisema vikosi vya Rwanda viliunga mkono M23 huko Goma kauli iliyopingwa na kukanushwa na Rwanda.