Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imetenga kiasi cha shilingi milioni 466 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuwawezesha kiuchumi makundi haya maalum.
Akikabidhi hundi kwa wanufaika wa mikopo hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisisitiza kuwa serikali inatarajia wananchi kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kupitia fursa hii. Aliwahimiza wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kufanya marejesho kwa wakati.
"Ikitokea mmezitumia fedha hizi kinyume na malengo yaliyokusudiwa, mtakuwa mmekwenda kinyume na dhamira ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na kamati ya uhakiki wa mikopo. Hakikisheni mnazitumia kwa lengo la kuinua biashara zenu na kufanya marejesho kama inavyotakiwa," alisema Mangosongo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri, Juma Salum, aliwataka wanufaika kuhakikisha wanazingatia taratibu za kisheria katika uendeshaji wa biashara zao, ikiwa ni pamoja na kulipa leseni za biashara na ushuru, ili kuwezesha wananchi wengine kupata mikopo kama hiyo.
Wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya wananchi, huku wakiahidi kuwa waaminifu katika marejesho.
"Kabla ya kupata mkopo, biashara yangu ilikuwa ndogo sana. Nilipopata taarifa kuhusu mikopo hii, nilihamasika kuomba, nikaweza kupata na kurejesha kwa wakati. Sasa nimeomba tena ili niendelee kukuza biashara yangu," alisema Haji Mwarabu, mfanyabiashara wa samaki mwenye ulemavu kutoka Kata ya Kanga, Bweni.
Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imetangaza kuwa dirisha la pili la uombaji wa mikopo ya asilimia 10 litafunguliwa kesho, na wananchi wanahamasishwa kujitokeza ili kufaidika na fursa hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED