MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameshauri serikali kuitisha Bunge la dharura kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi, akisisitiza msimamo wa chama hicho wa ‘hakuna uchaguzi bila mabadiliko'.
Vilevile, chama hicho kimetoa mapendekezo matatu kwa serikali kukabili mabadiliko ya kisera kwenye misaada katika sekta ya afya yaliyofanywa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Lissu alisisitiza msimamo huo jana mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, wilayani Kinondoni.
Lissu alisema kuna Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, lakini kwao CHADEMA, kama hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi. Lakini haina maana watasusia uchaguzi.
"Tusijaribu kuitanua lugha kuliko maana yake ya kawaida, hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi. Lazima tuzungumze hayo mambo mawili tuone tunawezaje tukaenda nayo mbele aidha kwa pamoja au kuamua lipi muhimu.
"Sasa hilo sitaki nizungumze hapa, zaidi tunakwenda kujifungia kisha tutaamua kwa pamoja ili uwe uamuzi wa chama na si wangu peke yangu. Tutakwenda kuonana na marafiki zetu duniani tuwaambie msimamo wetu hadharani. Tutawaomba watuunge mkono, na wale wasiotupenda tutawaangalia usoni, tutawaambia msimamo wetu ni huu," Lissu alisema.
Mtaalam huyo wa sheria alisisitiza msimamo huo wa ‘no reforms na election’ siyo wake, bali ni wa chama na kwamba kazi yake ni kutekeleza maagizo ya chama.
Kwa mujibu wa Lissu, chama hicho hakiwezi kwenda kwenye uchaguzi ambao alisisitiza kuwa kuingia katika uchaguzi kwa hali ya sasa ni kukubali kunyolewa au kuwa kama kondoo anayepelekwa machinjioni.
"Tunazungumzia kupata mageuzi kwa shuruti kama walivyopata Kenya, Malawi, Bunge letu linaweza kukaa muda wowote hata bila kuwa na ratiba," alisema Lissu
Alikumbushia kipindi cha nyuma Bunge liliwahi kuitishwa kwa dharura siku ya Jumamosi kuidhinisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika ukumbi wa Karimjee, na Muungano mpaka leo upo, hivyo kwa suala la katiba haiwezi kuwa ajabu.
Lissu pia alisema wafuasi wote wa chama hicho watakuwa na haki sawa kulingana na uwezo na kukitumikia chama, na kwamba waliokuwa timu Lissu wasitarajie upendeleo na timu Mbowe kuumizwa, bali wote watakuwa na haki sawa.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche alisema wamejipanga kufanya kazi kikamilifu huku wakilitaka Jeshi la Polisi kuacha kuwatishia kwa kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema chama hicho chini ya viongozi wapya na wastaafu, watajifungia ndani kwa muda wa wiki moja kwa ajili ya kuja na mkakati wa pamoja kuelekea uchaguzi.
Pia aliwataka wana-CHADEMA kote nchini kuachana na tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na badala yake wasonge mbele kwa nguvu ya pamoja kufanikisha agenda ya mageuzi.
Kuhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutoonekana wakati wa makabidhiano ya ofisi, Mnyika alisema katiba ya chama hicho inaruhusu Katibu Mkuu kusimamia zoezi hilo na kwamba hakuna shida kama watu wanavyodhani.
SERA ZA TRUMP
Wakati huo, CHADEMA imetoa mapendekezo matatu kwa serikali kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha misaada kwa sekta ya afya.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Wananchi CHADEMA, Ashura Masoud, lazima hatua zichukuliwe kukabili mabadiliko hayo.
Chama hicho kimependekeza serikali kuandaa mkakati wa dharura wa kisera na kibajeti wa kuhakikisha inakuwa na fedha za kutosha kwenye Mfuko wa Kudhibiti UKIMWI na Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI kwa kubana matumizi na kutenga vyanzo maalum na vya lazima katika bajeti ya taifa, ili kupunguza makali ya uhaba wa fedha za ARV na UKIMWI.
Pia Bunge linaloendelea sasa kujadili ajenda ya dharura, serikali iwasilishe taarifa ya tathmini na mkakati wa kina wa namna ya kukabiliana na upungufu wa fedha katika sekta ya afya na nyingine za maendeleo kisha litokea na azimio.
"Rais Samia Suluhu Hassan na wakuu wenzake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU) wafanye mkutano kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi mpana na wa kina zaidi kupata vyanzo mbadala vya fedha na kuziba pengo la kibajeti linalosababishwa na Marekani kusitisha misaada ya maendeleo," alishauri.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya fedha zinazotumika katika eneo hilo ni kutoka nje ambapo Mpango wa Dunia wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) unachangia asilimia 40 katika kapu hilo na michango ya mashirika mengine kama WHO, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) na Global Fund.
"Idadi ya waathirka wa VVU hadi sasa wanaonufaika na misaada ni takribani milioni 1.5, na wastani wa Sh. bilioni 204 kwa mwezi hutumika," alisema.
Aliongeza: Tathmini iliyofanywa na Kamati ya Afya ya Bunge la Wananchi imebaini kusitishwa kwa misaada hii kutaathiri huduma ya ARVs pamoja na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI KWA asilimia 50."
Nipashe ilimtafuta Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, ambaye kupitia msaidizi wake, alisema suala hilo litatolewa ufafanuzi baada ya kuzungumza na wakubwa wa nchi kisha kutolewa taarifa kwa umma na si mwandishi mmoja mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED