Wananchi wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na mradi maji kwa asilimia 100 na kuondokana na magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Mradi huo unatekelezwa na shirika la water aid la Uingereza kwa kushirikiana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoani Manyara.
Akizungumza katika mkutano wa ushirikishwaji wa wadau mjini Katesh, Mkuu wa miradi wa water aid Tanzania, Beda Levira amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.
Levira amesema waterAid katika kutekeleza mradi wa mfano Hanang' utatatua changamoto ya maji safi, vyoo bora na usafi wa mazingira na utanufaisha wakazi wengi wa vijiji 96 wa kata 33 za wilaya ya Hanang' .
"Watu watapata maji kwa asilimia 100 na kuondokana na changamoto ya magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji," amesema Levira.
Mhandisi wa maji kutoka Ruwasa, Barnabas Taligunga, amesema mradi huo utaongeza nguvu ya uboreshaji wa usafi wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwa watumiaji ili kudhibiti uwezekano kusambaa magonjwa kipitia maji.
"Mradi huu wa mfano kwa hapa Tanzania unafanyika Hanang' pekee hivyo wilaya nyingine zitapaswa kuja kujifunza utekelezaji wa mradi huu," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, mganga mkuu wa mkoa, Dk. Andrew Method ametoa wito kwa viongozi wa Hanang' kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waterAid kutekeleza mradi huo ili uwe mfano kwa wilaya nyingine.
"Hatuna budi kumshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mradi huu kufanyika Manyara, hususani wilayani Hanang' kwani ni mradi wa mfano na utasaidia kutatua changamoto mbalimbali hususani za afya," amesema Dk Method.
Mkurugenzi Mtendaji wa Programu za Kimataifa (IPD), WaterAid UK, Amaka Godfrey, amesema watashirikiana na serikali kuhakikisha mradi huo unawanufaisha wananchi wengi zaidi katika kupata maji safi na salama.
Amesema mbinu iliyotumika ya kuifikia Wilaya hiyo nzima ni nzuri na yeye ameona ikifanya vizuri katika nchi nyingine.
Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Hanang' wamesema kuwa wataulinda mradi huo ili uweze kuwanufaisha wao na kizazi kijacho.
Mmoja kati ya wakazi hao Isack Mayomba amesema wanawashukuru viongozi waliofanikisha mradi huo kutekelezwa wilayani Hanang'.
"Mwaka 2023 tulipatwa na matatizo hapa Hanang' na leo 2025 tumepata mradi huu, ni jambo la kumshukuru Mungu kwani amezidi kutufuta machozi," amesema Mayomba.
Mradi huu utakapokamilika, Hanang' itatumika kama mfano kwa wilaya nyingine nchini katika kujifunza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED