Ubovu wa barabara inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga umekuwa kero kwa watumiaji wake, hususan madereva wa magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji). Uharibifu wa vyombo hivyo vya usafiri umekuwa ukiwagharimu wamiliki wake fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo.
Baadhi ya madereva wameeleza kuwa barabara hiyo mbovu ni changamoto kubwa kwao, kwani vyombo vyao vya usafiri huharibika mara kwa mara na kuwasababishia hasara kubwa.
John Mabele, dereva wa gari la wagonjwa (ambulance) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, anasema ubovu wa barabara hiyo ni mzigo kwa serikali kwa sababu magari ya wagonjwa yanaharibika mara kwa mara.
“Barabara inapokuwa na mashimo, siyo rafiki kwa vyombo vya moto. Vimekuwa vikiharibika vitu vingi hasa shock absorbers, na tunapovipeleka kwa ajili ya matengenezo hutumia gharama kati ya shilingi milioni 2 hadi milioni 3,” anasema Mabele.
Anatoa wito kwa serikali kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kupunguza gharama kubwa za matengenezo ya magari ya wagonjwa, hasa kwa kuzingatia kuwa magari hayo hutakiwa kusafiri kwa mwendo wa haraka ili kuwaokoa wagonjwa.
Kwa upande wake, dereva wa bajaji, Tasiri Kassimu, anasema barabara hiyo mbovu inawasababishia hasara kubwa kutokana na mashimo mengi yaliyopo. Anaeleza kuwa mtikisiko unaosababishwa na hali mbaya ya barabara hiyo huharibu miguu ya bajaji, vikombe, sliders, na mfumo wa umeme.
“Kila baada ya muda mfupi lazima tufanye matengenezo. Tunatumia kati ya shilingi 200,000 hadi 300,000 kwa ajili ya vipuri pekee, bila kujumlisha gharama za fundi, ambazo zinaanzia shilingi 30,000 au zaidi, kutegemea kiwango cha uharibifu,” anasema Kassimu.
Anabainisha kuwa bajaji inapoharibika, lazima aitengeneze kila baada ya wiki moja au mbili, jambo linalomfanya kufanya kazi bila faida.
Dereva mwingine wa bajaji, Sayi Kitula, anasema kuwa gharama za usafiri kutoka Stendi ya Mabasi ya Mkoa hadi Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga kwa mgonjwa ni shilingi 10,000 kwa safari ya kukodi, lakini abiria wa kawaida hulipa shilingi 1,000 kwa kichwa.
“Hata hivyo, tunalazimika kutumia zaidi ya shilingi 200,000 kwa matengenezo kila mwezi. Ukilinganisha na kipato chetu, ni mzigo mzito sana,” anasema Kitula.
Fundi wa bajaji, Faraja Abdul, anasema kwa siku moja hupokea zaidi ya bajaji tano zinazohitaji matengenezo kutokana na ubovu wa barabara hiyo. Anaeleza kuwa sehemu zinazoharibika zaidi ni miguu ya bajaji, sliders, shock absorbers, na vikombe.
“Kwa matengenezo, gharama ya chini kabisa ni shilingi 150,000 hadi 200,000, huku pesa ya ufundi ikiwa kati ya shilingi 30,000 hadi 50,000, kutegemea kiwango cha uharibifu,” anasema Abdul.
Anasema kuwa, ingawa kama fundi anafaidika na uharibifu huo kwa kupata kazi, hawezi kufurahia hali hiyo kwa sababu barabara hiyo ni muhimu kwa kusafirisha wagonjwa.
MSIMAMO WA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA SHINYANGA
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, anasema kuwa amekuwa akilalamikia ubovu wa barabara hiyo kwa muda mrefu, hata kwa maandishi, lakini hakuna utekelezaji wowote wa ahadi zinazotolewa.
“Barabara hii ni mbovu sana. Mimi mwenyewe sasa hivi situmii gari langu kuja ofisini kwa sababu naogopa litaharibika. Tuna gari moja ambalo tumelipaki baada ya kushindwa kupata fedha za matengenezo,” anasema Dk. Luzila.
Januari 18, 2023, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, alipofanya ziara mkoani Shinyanga na kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, aliahidi kujengwa kwa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 5.8 ili kuunganisha hospitali hiyo na wananchi.
Wananchi walipewa matumaini kupitia ahadi hiyo, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote uliofanyika, hali inayoongeza mateso kwao.
SERIKALI YATOA AHADI MPYA KWA UJENZI WA BARABARA
Mratibu wa Ujenzi wa Miundombinu ya Afya Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu, anasema kuwa sera ya afya inaelekeza kuwa barabara zinazounganisha jamii na hospitali zinapaswa kushughulikiwa kwa kushirikiana na mamlaka za ujenzi wa barabara, kama Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha miundombinu ya usafiri inakuwa rafiki kwa wagonjwa. Tumekuwa tukishirikiana na TARURA ili kuhakikisha barabara hii inakarabatiwa,” anasema Mlyutu.
Sera ya Afya ya mwaka 2007, kifungu namba 4:3:1 kipengele cha (vi), kinasisitiza kuwepo kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma, binafsi, mashirika ya dini, asasi za kijamii, na mamlaka zingine katika kutoa huduma bora za afya.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Samson Pampili, anasema kuwa kupitia fedha za Benki ya Dunia, barabara mbili zitajengwa kwa kiwango cha lami ili kumaliza tatizo hilo.
“Barabara ya kwanza ni ya kutoka Nguzonane hadi Mwawaza, yenye urefu wa kilomita 4.2, ambayo inapita katika hospitali hiyo. Barabara ya pili ni ya kutoka Shinatoni, inayopita Ndala, yenye urefu wa kilomita 1.6. Wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka Kituo cha Afya Kambarage wataweza kupita katika barabara hiyo na kuwahi kupata matibabu,” anasema Pampili.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu, anasema kuwa ubovu wa barabara hiyo umekuwa ukimuumiza kichwa, lakini tatizo hilo litamalizika kwa sababu tayari wamepata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Ubovu wa barabara ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga umekuwa changamoto kubwa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na wagonjwa wanaohitaji huduma za afya haraka.
Ingawa serikali imeahidi kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, wananchi wanasubiri utekelezaji wa ahadi hiyo ili kupunguza mzigo wa gharama za matengenezo na kuhakikisha usafiri wa wagonjwa unakuwa wa haraka na salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED