“Baba wa mtoto njiti kupumzika siku saba, Mama likizo baada ya wiki ya 40"

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 05:03 PM Jan 31 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Madini Anthony Mavunde.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amesema likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti itajumuisha na muda uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito na Baba atapewa siku saba za mapumziko.

Mavunde ameyasema hayo leo Januari 31,2025 bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha maelezo ya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024 (The Labour Laws (Amendments) Bill, 2024) zinazolenga kuleta ustawi katika sekta ya kazi nchini, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.

Amesema kifungu kipya cha 34A kinalenga kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30 ili kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza. 

"Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kimebainisha aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum" amesema Mavunde.

Katika kifungu cha 37, Mavunde amesema kimeweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi ili kuzuia uingiliaji wa mchakato kushughulikia migogoro.

"Kifungu cha 71 kimeweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma" amesema Mavunde.

Aidha, Mavunde amesema kifungu cha tisa cha Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 kimeweka masharti ya kumtaka Raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi badala ya kibali kingine cha kazi.

Kliki kusoma habari hii inayohusiana