Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga limepitisha makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni 64.6 kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Bajeti hiyo ilipitishwa juzi katika kikao cha Baraza maalumu la Madiwani katika Mji wa Mkuranga, ambapo pia walishukuru Serikali kwa kutenga na kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati.
Akisoma makadirio ya bajeti hiyo, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mkuranga, Grace Mwaigaga, alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka ukilinganisha na ya mwaka 2024/2025, ambapo bajeti ya mwaka huo ilikuwa shilingi bilioni 64.2.
Mwaigaga alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri inakadiria kukusanya shilingi bilioni 15.8 kutoka vyanzo vyake vya ndani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.6 ikilinganishwa na mwaka 2024/2025, ambapo vyanzo vya ndani vilikusanya shilingi bilioni 14.3.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga, Waziri Kombo, alisema kuwa miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2024/2025 imefanikiwa kutekelezwa kwa asilimia 51, huku akishukuru kwa kuongezeka kwa fedha za Serikali kuu zilizopangwa kufika kwa wakati.
Kombo alisisitiza kuwa bajeti ya mwaka ujao imezingatia vipaumbele vya Halmashauri katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu na barabara, na maeneo yenye changamoto yatatatuliwa kupitia bajeti hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omari Mwanga, aliwakumbusha Madiwani kujenga ushirikiano bora katika kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao, ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila vikwazo.
Mwanga pia alisisitiza wazazi na walezi ambao bado hawajawapeleka watoto wao shuleni kuhakikisha wanawapeleka na kuwafuatilia maendeleo yao, ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kwani Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED