Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika hivi karibuni umemtaka Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi, kukaa meza moja na wanamgambo wa M23 kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja ili kutafuta suluhu ya amani katika taifa hilo.
Taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Mkutano huo, ambaye pia ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (Twitter), ilieleza kuwa viongozi hao walikutana Januari 29, chini ya uenyekiti wa Rais wa Kenya, William Ruto, kujadili hali ya usalama nchini DRC.
Miongoni mwa makubaliano ya mkutano huo ni pendekezo la Rais Tshisekedi kushiriki mazungumzo na kundi la M23. Kadhalika, viongozi hao walikubaliana kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inapaswa kuitisha mkutano wa dharura na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo.
Museveni aliambatanisha taarifa hiyo na orodha ya viongozi waliohudhuria mkutano huo, wakiwemo Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa Somalia Hassan Mohamud, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, Rais wa Rwanda Paul Kagame, na mwenyeji wao, Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Viongozi hao walilaani hali inayoendelea nchini DRC na kutuma salamu za rambirambi kwa wananchi wa DRC waliopoteza maisha katika machafuko hayo. Pia, walieleza masikitiko yao kuhusu mateso wanayokumbana nayo raia wa kawaida, hususan wanawake na watoto.
Hata hivyo, pendekezo hilo la mazungumzo limetupiliwa mbali na Serikali ya DRC kupitia Waziri wa Ulinzi, Guy Kabombo, ambaye alisisitiza kuwa mazungumzo na waasi wa M23 hayawezekani.
"Nimeamuru kwamba mipango na maagizo yote yanayohusiana na mazungumzo yanayodaiwa kufanywa na magaidi wa M23 yateketezwe kabisa mara moja," alisema Kabombo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED