Kiongozi wa Muungano wa Mto Kongo (AFC), Corneille Nangaa, amesema kuwa kundi hilo halipiganii madini wala rasilimali yoyote katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), bali linahitaji kurejesha heshima na utawala bora nchini humo.
Nangaa alitoa kauli hiyo Januari 30, 2025, katika mkutano wake mjini Goma, akieleza kuwa kundi hilo lipo tayari kufanya mazungumzo na serikali kama sehemu ya mipango yake ya kupata mamlaka ya kisiasa.
Hata hivyo, Rais wa DRC, Fèlix Tshisekedi, alikataa wito huo, akisisitiza kuwa serikali yake haipo tayari kufanya mazungumzo na kundi la kigaidi. Waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, wamesema kuwa baada ya kuuteka mji wa Goma, sasa lengo lao ni kuushambulia na kuuteka mji mkuu, Kinshasa.
Ripoti zinaonyesha kuwa kundi hilo linaendelea na mapigano na kuelekea Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa katika DRC, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano. Nangaa alidai kuwa kundi hilo linapigana kwa sababu tatu, akisema kwamba utawala wa Tshisekedi umeharibu jeshi, polisi, na haki nchini DRC.
Tangazo la kundi hilo limekuja baada ya Rais Tshisekedi kutangaza kuandaa jeshi kubwa kupinga uasi huo. Nangaa alisema, "Namtia moyo Tshisekedi aendelee kupigana, lakini tutapambana naye hadi tufike Kinshasa." Alisisitiza kuwa mapigano yao siyo ya kutafuta rasilimali, bali ni kwa ajili ya kurejesha hali nzuri na kutoa msaada kwa watu wa DRC.
Waasi hao walitoa wito kwa wakazi wa Goma kuendelea na maisha yao ya kila siku wakati waasi wakifanya kazi ya kusaidia misaada ya kibinadamu inayohitajika sana. Goma, ambayo ni kitovu muhimu cha kibinadamu, inahudumia zaidi ya watu milioni mbili waliokimbia makazi yao kutokana na vita.
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa waasi hao wanaungwa mkono na wanajeshi kutoka Rwanda na kwamba mapigano yameathiri huduma za kimsingi katika mji wa Goma. M23 ni moja ya makundi zaidi ya 100 yenye silaha yanayopigania udhibiti wa eneo la mashariki la Kongo, lenye utajiri wa madini, kwa zaidi ya muongo mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED