MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imeirudisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesi ya mwanasiasa mkongwe Dk. Wilbroad Slaa , huku ikielekeza suala la dhamana ya mshtakiwa kupewa kipaumbele.
Kukiwa na agizo hilo la Mahakama Kuu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ajitosa kumtetea Dk. Slaa baada ya jana kujitambulisha mbele ya Jaji Arnold Kirekiano wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kwamba anamwakilisha mshtakiwa huyo.
Dhamana kwa mwanasiasa huyo ilizuiwa tangu Januari 10 mwaka huu alipofikishwa mahakamani, hivyo kuendelea kusota kwenye Gereza la Keko, Dar es Salaam.
Dk. Slaa alifungua kesi ya mapitio ya kesi yake katika Mahakama Kuu, akipinga mwenendo wa Mahakama ya Kisutu kuahirisha usikilizwaji dhamana yake kutokana na maombi ya kuipinga yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka.
Maelekezo hayo yaliyotolewa jana na Jaji Arnold Kirekiano wa mahakama hiyo, aliyesema kuwa kesi ya msingi iko katika Mahakama ya Kisutu ambayo ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo kuamuru kesi irudishwe huko ili itolewe uamuzi kwa sababu ilishafika kwenye uamuzi.
Jaji Kirekiano pia alieleza kuwa shauri namba 1637/2025 ni maombi yanayohusu zuio la dhamana lililotolewa na upande mashtaka Januari 10, 2025 katika shauri namba 993/2025 lililoko Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki.
Jaji Kirekiano alisema kuwa katika maombi hayo, mpeleka maombi alikuwa na hoja saba ambazo aliziwasilisha mahakamani huko kupitia jopo la mawakili wa utetezi.
Alisema kuwa katika hoja zilizowasilishwa na Wakili Hekima Mwasipu, alidai wanaomba mahakama ipitie jalada la shauri 1015/2025 liliko mbele ya Hakimu Nyaki kwa kuwa hana ujuzi kwenye kuliendesha.
Pia alidai mpeleka maombi wao alipelekwa kwenye Gereza la Keko kinyume cha sheria, pia walidai kuwa mwenendo wa uendeshwaji kesi hiyo, Januari 10 na 13, 2025 ulikuwa na mazingira ya uzembe na upendeleo ambao kimsingi ulifanya uhuru wa mpeleka maombi kubebwa na mahakama.
Aliendelea kudai kuwa mwenendo wa uendeshwaji shauri hilo kwa tarehe tajwa ulikuwa si sahihi, pia waliomba mahakama hiyo ieleze kuwa shauri lolote linalohusu uhuru wa mshtakiwa lipewe kipaumbele kuliko mashauri yoyote yale, pia walidai kuwa maofisa wa mahakama wameendesha mashauri kwa kukiuka kanuni.
Jaji alisema kuwa maombi hayo yalikuwa sawasawa mahakamani hapo na msingi wake mkubwa ni malalamiko dhidi ya maahirisho katika Mahakama ya Kisutu na alipitia hoja za pande zote mbili.
Pia alisema mpeleka maombi na mawakili wake walijikita katika hoja kwamba kuna ukiukwaji utoaji haki kwa mshitakiwa kwa kutopewa haki ya kupewa dhamana kwa kuwa shtaka lake linadhaminika.
Alisema anakubaliana na msingi wa hoja ya kwamba suala la utoaji haki katika shauri ni wajibu wa mahakama kama ilivyotolewa na mlalamikaji.
Alisema katika utaratibu wa kawaida, mahakama hiyo ilipaswa kuamua kuhusiana na hatma ya mshtakiwa, lakini Upande wa Jamhuri ulikuwa na jambo lingine na hapo ndipo walipofungua maombi kwa ajili ya kuzuia mshtakiwa kupewa dhamana.
Jaji alisema kwa hoja ya wakili wa mpeleka maombi ni kwamba maahirisho yaliyofanyika Januari 13 hadi 23, 2025 hayakuwa sawa kwa kuahirisha shauri la dhamana kwa hoja ya kuwa na mrundikano wa mashauri.
Alisema dhamana ya mshtakiwa ni suala la haki ambayo linaleta maana kwenye dhana ya kwamba kila mtu hana kosa hadi pale itakapothibitika kuwa ametenda kosa, hivyo mambo yanayohusiana na hoja ya dhamana yanapaswa kufanyika siku ya kwanza mshtakiwa atakapofikishwa mahakamani.
Alisema panakuwapo pingamizi dhidi ya dhamana, basi hilo ni pingamizi dhidi ya haki ambalo linagusa uhuru wa mtu binafsi na kama mahakama itapaswa kusubiri, jambo hilo linapaswa kuwa la dharura zaidi. Pia maahirisho ya Januari 13 hadi Januari 23, 2025 hayakuwa ya msingi.
Alisema anamini maelezo hayo yatasaidia kuweka viwango katika mashauri kama hayo kwa siku zijazo.
Alieleza kuwa maombi kwenye hoja ya pili ambayo msingi wake ulikuwa unamgusa hakimu mwenyewe yanayohusu na suala la umahiri wa hakimu mahakama, si mahala pake na kusisitiza kuwa kila shauri lina mahali pake.
"Mahakama imezingatia mwenendo huu lakini haina mamlaka ya kubatilisha uhalali wa hati hiyo ya mashtaka kwani suala hilo linatakiwa kushughulikiwa na mahakama husika ambayo ni Mahakama Kisutu katika hatua ya kwanza," alisema.
Alisema hoja ya kushawishi mahakama hiyo kutolea uamuzi suala ambalo linasubiri uamuzi katika mahakama nyingine ni kuleta mkanganyiko, hivyo alielekeza uamuzi wa hoja ya uhalali wa mashtaka na dhamana itolewe katika Mahakama Kisutu.
Dk. Slaa anashtakiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X.
LISSU AJITOSA
Jana Lissu alijitambulisha Mahakama Kuu kabla ya jaji kutoa uamuzi wa mashauri mawili yaliyofunguliwa na Dk. Slaa kwa kushirikiana na jopo la mawakili wake kwa wakipinga mwenendo wa kesi ya tuhuma za kusambaza taarifa za uongo iliyoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kabla ya uamuzi huo kutolewa, Lissu akiwa kwenye benchi la mawakili wa utetezi, alisimama na kutambulisha jopo lote kwa sababu yeye ndiye alikuwa wakili mkuu (senior Advocate), akidai wote wanamwakilisha mshtakiwa.
Mawakili wengine wanaomwakilisha Dk. Slaa ni Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Sanga Melikiole, Sisty Aloyce, Edson Kiratu na Mwanaisha Mdeme.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED