Jengo la TRA lawaka moto Kariakoo

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:57 AM Jan 31 2025
Jengo la TRA lawaka moto Kariakoo.

JESHI la Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kuuzima moto uliokuwa ukiteketeza jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo baada ya kufika eneo la tukio, alisema haijulikani moto huo ulianza kuwaka muda gani japo juhudi za uokozi zinaendelea.

Alisema Jeshi la Uokoji, magari ya Zimamoto yameshafika katika eneo hilo na shughuli ya kuuzima ilikuwa ikiendelea.

“Bado hatujabaini nini chanzo cha moto huu, na kwa sasa siwezi kusema chochote mpaka pale tutakapofanikiwa kuudhibiti kwa sababu vyombo vyote vya dola viko hapa,” alisema Kayombo.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema janga hilo lilikuwa nje ya uwezo wao na kwamba watakaa na kutathmini chanzo na kuchukua hatua.

Alisema jengo lililoathirika zaidi ni ghorofa ya tano ambalo lilikuwa na baadhi ya nyaraka na ukumbi wa mikutano. 

"Tunafanya juhudi za haraka ili walipa kodi wasipate shida yoyote kutokana na janga hili, kwa sababu taarifa nyingi muhimu zilikuwa hazikai ghorofa hilo ambalo limeathiriwa na moto," alisema Mwenda.  

Naibu Kamishna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Goodluck Zelote, alisema walipopata taarifa ya ajali hiyo haraka walipeleka mitambo ya kuzima moto.

"Mpaka sasa operesheni inaendelea tumefanikiwa kuuzima moto, lakini tutatoa taarifa kamili baada ya kumalizika kabisa kwa shughuli hii," alisema Zelote. 

Baadhi ya mashuhuda walisema walipoona moshi mkubwa unafuka katika ghorofa hilo, walitoa taarifa Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya uokozi.

Jabiri Mtulya, alisema moto huo haujaleta madhara makubwa kwa sababu ya kuwapo kwa vifaa vya kisasa vya uokozi. 

"Sidhani kama kuna aliyepata majeraha kwa sababu moto ulianza kidogo kidogo kwahiyo ilikuwa rahisi kwa wao kujiokoa," alisema. 

Shuhuda mwingine, Fatma Abubakari, alisema hajui chanzo, lakini anahisi hitilafu ya umeme huku akilipongeza Jeshi la Zimamoto kwa uharaka na kufanikisha uokozi kabla madhara hayajawa makubwa.

Abeli Mgonja, alisema kwenye majira ya saa sita mchana jengo hilo lilianza kuwaka moto ulioambatana na moshi mzito.  

“Tunashukuru kulikuwa na askari walikuwa doria wakaanza kuweka ulinzi, na kufanya taratibu za uokozi lakini kuna mmoja wa walinzi kampuni binafsi aliteguka mguu wakati tunahamisha vitu,” alisema Mgonja.