MOJA ya sakata lililogonga vichwa vya mashabiki wa wadau wa soka nchini kuanzia katikati ya wiki ni uamuzi wa kupewa uraia wa Tanzania kwa wachezaji wa Singida Black Stars inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Wachezaji hao ambao sasa wanatambulika ni raia wa Tanzania ni Emmanuel Kwame Keyekeh, Josephat Arthur Bada na Mohamed Damaro.
Ilianza juzi kama utani au vibonzo katika mitandao ya kijamii kama ilivyo kawaida, lakini baadaye klabu hiyo ilithibitisha ni kweli wachezaji wao Keyekeh aliyekuwa raia wa Ghana, Bada (Ivory Coast) na Damaro, aliyetokea Guinea, waliomba wenyewe uraia katika mamlaka husika.
Baadaye ikatoka taarifa kutoka kwa Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, akithibitisha kwa wachezaji hao kupatiwa uraia wa Tanzania.
Taarifa ilisema wachezaji waliomba na walipewa kwa mujibu wa vifungu vya 9, 23 vya Sheria ya Uhamiaji, sura ya 357.
"Kwa muktadha huo, Idara ya Uhamiaji inapenda kuutaarifu umma watajwa ni raia wa Tanzania kwa Tajnisi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Saa chache baada ya hapo, klabu ya Simba nayo ikatangaza kuandika barua kwenda idara hiyo, kuomba uraia wa wachezaji wake tisa wa kigeni.
Barua huyo iliyotumwa juzi na kusainiwa na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, ilisema inaomba wachezaji wake tisa wa kigeni wapatiwe uraia ili wafanye kazi kama Watanzania.
"Sababu ya maombi haya ni wachezaji hao bado ni vijana, hivyo wana muda mrefu wa kuitumikia Tanzania, zaidi wanaweza kuwa chachu ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini," ilieleza barua hiyo.
Ina maana hata klabu ya Simba inaona kama ni vigezo ambavyo wachezaji wa Singida Black Stars wamevitimiza na kupewa uraia, basi wachezaji wao hawawezi kuvikosa.
Turudi sasa kwenye mada yenyewe. Tujiulize, hivi ni kweli wachezaji hawa wamebadilishwa kwa sababu ya kuisaidia Tanzania, labda kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars), hapo baadye?
Hivi ni kweli wachezaji hawa wana uwezo wa hali ya juu mno wa kuweza kuisaidia Stars kuliko hawaliopo? Maana kuna kipengele cha kuwapa uraia watu ambao ni wataalam wa hali ya juu na vipaji vikubwa visivyo na shaka hata kidogo.
Tunaendelea kujiuliza. Je, ina maana Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco, ameomba wachezaji hawa wajumuishwe kwenye kikosi hicho baada ya kujidhihirisha wana vipaji maalum?
Kama si hivyo, Morocco asiporidhika nao na kutowaita kwenye kikosi cha Taifa Stars, watanyang'anywa uraia? Tuna uhakika mpaka kufikia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) na AFCON, wachezaji hawa watakuwa katika kiwango kinachotakiwa cha kuichezea Stars.
Je, suala hili kweli limefanywa kwa ajili ya manufaa ya taifa au klabu ya Singida Black Stars? Kwa nini wachezaji walioomba uraia wawe kutoka klabu moja tu? Binafsi zipingi wachezaji kuomba na kupewa uraia. Lakini 'uspesho' na uharaka huu ndio unaowashangazwa wadau wa soka nchini.
Angalau angepewa mtu kama Bernard Morrison ambaye amekuwa akihangaika usiku na mchana kuomba uraia bila mafanikio wengi wangeweza kuelewa kwa sababu mashabiki wa soka wanajua kiwango chake. Ni mmoja ya wachezaji wenye kipaji cha hali ya juu mno, ambaye hata angepewa hakuna ambaye angeshangaa. Huyu mmoja tu anaweza kukibadilisha kikosi cha wachezaji 11 uwanjani kikawa moto, kutokana na uwezo wake wa kuwachanganya mabeki, akili na kasi, chenga za maudhi, hivyo nchi inaweza kunufaika na kipaji chake.
Kwa vyovyote vile, mlango huu ambao umefunguliwa unaweza kuleta shida baadaye, kwa sababu tunaweza kusikia Yanga, Azam, Tabora United, Coastal Union, nao wakaomba uraia kwa wachezaji wake kwa kipengele kile kile cha Tajnisi.
Na watasema ni kwa ajili ya manufaa ya taifa, lakini kumbe ni klabu zao na wachezaji wengi wa kigeni katika kikosi kwa kisingizio hicho.
Ifike wakati siasa iachwe kwenye soka, wachezaji wapate uraia kwa manufaa kweli ya nchi na isionekane kweli ni kwa ajili hiyo, siyo kuzisaidia klabu na kusingizia nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED