SERIKALI imesema ili kuwapunguzia wananchi adha ya foleni wakati wa mkutano wa viongozi wa Afrika unaonza kesho, wageni watakuwa wakitumia njia ya mwendokasi kwenda na kurudi Uwanja wa Ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema abiria wanaokwenda na kurudi kutoka mjini wataendelea kutumia barabara ya kawaida.
“Nchi yetu imepata bahati ya ugeni mkubwa kuanzia kesho kutokana na Mkutano wa Afrika wa Masuala ya Nishati. Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametupa heshima kubwa kama taifa kuleta viongozi wa Afrika na Dunia kuja kwetu.
"Sasa ili kuounguza adha kwa wananchi, serikali yenu umeamua wageni watumie njia ya Mwendokasi wakitoka na kwenda Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na wananchi waendelee kutumia barabara ya kawaida," amesema.
Katika hatua nyingine, Ulega amekagua maandalizi ya kimiundombinu ya mkutano huo, ikiwemo kufungwa kwa taa za mwanga barabarani ambazo zimeanza kubadili mwonekano wa jiji la Dar nyakati za usiku.
Mkutano wa Nishati wa Bara la Afrika utakutanisha viongozi wakuu wa Afrika kujadili namna ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa Afrika utafanyika kati ya Januari 27 na 28 mwaka huu.