Wana VICOBA washauriwa kujisajili kisheria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:48 AM Jan 26 2025
Wana VICOBA washauriwa kujisajili kisheria
Picha: Mtandao
Wana VICOBA washauriwa kujisajili kisheria

SERIKALI imetoa rai kwa wananchi kuhakikisha vikundi vya huduma ndogo vya fedha vinavyojulikana kama VICOBA vinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2028.

Kwa kufanya hivyo, watawezeshwa kujikwamua kiuchumi, kupata mikopo katika taasisi za fedha na kuondokana na changamoto za kiutendaji.

Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, wakati timu ya maofisa kutoka Wizara ya Fedha iliyoambatana na maofisa kutoka taasisi za Wizara ya Fedha na watoa huduma za fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha zilizo rasmi katika ukumbi wa Ofisi ya Tarafa ya Mbulumbulu, wilayani hapa.

Kibakaya alisema vikundi vya huduma ndogo za fedha vinavyotumiwa na wananchi katika maeneo mengi mjini na vijijini ni muhimu kusajili ili kuweza kutambulika kisheria na kupata fursa mbalimbali katika halmashauri na taasisi za fedha.

‘‘Usajili wa vikundi vya huduma ndogo za fedha ni muhimu sana na unafanyika kwa njia ya mfumo. Mwana  kikundi anaweza kujisajili bila kwenda ofisi ya halmashauri. Mfumo  unaotumika unaitwa "WEZESHA PORTAL" pia halmashauri zote nchini wako waratibu wa huduma ndogo za fedha ambao watawasajili kupitia mfumo huo” alisema.

Kibakaya alisisitiza kuwa usajili wa vikundi vya huduma ndogo za fedha utawawezesha pia kunufaika na mikopo ya halmashauri ya asilimia kumi inayotolewa na Serikali ambayo imeanza kutolewa ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Ofisa Sheria Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhani Myonga, alisisitiza wananchi kusoma mikataba ya mikopo ili kujua masharti ya mikataba na utekelezaji wake na kuwa na uhakika wa urejeshaji wa mkopo ili kuepuka migogoro na watoa huduma.

Aidha, alisisitiza wananchi kuzingatia kiwango cha mkopo wanachopokea kilingane na kiwango kilichoandikwa katika mkataba, kufahamu riba ya mkopo, aina ya urejeshaji na kufahamu adhabu ya kuchelewesha kurejesha mkopo kabla ya kusaini mkataba.

‘Ni muhimu kuhakikisha mkataba una kipengele kinachotoa fursa ya majadiliano juu ya marekebisho ya masharti ya mkataba ikiwemo kuongezewa muda wa marejesho ili kumpatia nafuu ya marejesho tofauti na awali endapo mkopaji atapata changamoto itakayosababisha kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati,’ alisisitiza Myonga.

Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Karatu, Joshua Mwamsojo, alisema mafunzo hayo yatawezesha wananchi kufuata Sheria na taratibu za namna ya ukopaji, ili kuepukana na mikopo isiyo rasmi.

‘‘Naipongeza serikali kwa mafunzo haya na nitoe rai mafunzo haya yawe endelevu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusaidia kuondokana na changamoto za fedha. 

“Natoa wito kwa wananchi wa wilaya ya Karatu waepuke kukopa katika taasisi zisizo rasmi, watumie elimu waliyoipata katika kupanga matumizi ya fedha wanazopata na nina Imani yatawasaidia kujikwamua kiuchumi dhidi ya umaskini,” alisisitiza.

Maeneo yaliyofikiwa katika wilaya ya Karatu ni pamoja na Kata ya Karatu Mjini, Tarafa ya Endabash (Kata za Kansay, Buger na Endabash), Tarafa ya Eyasi (Kata za Mang’ola na Baray) na Tarafa ya Mbulumbulu (Kata za Rhotia na Mbulumbulu).

Baada ya kuhitimisha programu , timu hiyo ya wataalam inaendelea na programu katika wilaya za Ngorongoro na Longido.