Mayanga afunguka kupata tuzo, kuipandisha Mbeya City

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:43 AM Jan 27 2025
Salum Mayanga, kocha timu ya Mbeya City
Picha: Mtandao
Salum Mayanga, kocha timu ya Mbeya City

BAADA ya kutangazwa kuwa Kocha Bora wa Desemba, kwenye Ligi ya Championship, , amezungumza kwa mara ya kwanza akisema tuzo hiyo imempa motisha na morali wa kuirudisha timu hiyo Ligi Kuu.

Mayanga, ambaye ni kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar, kwa sasa anainoa Mbeya City, majuzi akitangazwa kuwa kocha bora wa Desemba, huku mchezaji wa timu hiyo, Kilaza Mazoea, akitangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo.

"Nashukuru sana vijana wangu, viongozi, na wasaidizi wangu wa benchi la ufundi ambao wamenisaidia hadi kupata tuzo. Hii ina maana kubwa kwangu, itanisaidia sana kupambana kadri ya uwezo wangu ili niirudishe Mbeya City Ligi Kuu," alisema kocha huyo.

Mbeya City ilishuka daraja msimu wa 2022/23 ilipoduwazwa na timu iliyokuwa inachipukia, Mashujaa FC, ikichapwa jumla ya mabao 4-1 katika mchezo wa pili wa mchujo, baada ya kufunga mabao 3-1 ugenini, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kabla ya kukubali tena kipigo cha bao 1-0 nyumbani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Akizungumzia mzunguko wa pili ligi hiyo, alisema utakuwa mgumu kwani kila timu itakuwa imejipanga kisawasawa, lakini hiyo haizuii malengo yao waliyojiwekea msimu huu.

"Mzunguko wa pili utakuwa mgumu kimbinu na kiufundi, mategemeo yetu ni kucheza kama wa kwanza, ili kuongeza umakini, tutacheza kwa ari na kujituma, tunataka tushinde mechi nyingi zaidi.

Kwa upande wa usajili, umezingatiwa kwa asilimia 95, kilichobaki ni kwangu mimi na wasaidizi wangu kutengeneza muunganiko wa vijana waliokuwapo na wapya," alisema.

Timu hiyo inashika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi ya Championship, ikiwa na pointi 34 kwa michezo 15 iliyocheza, ikiwa nyuma kwa pointi saba kwa vinara, Mtibwa Sugar ambayo imekusanya pointi 41 mpaka sasa.