WAKAZI wa manispaa wako hatarini kukumbwa na maradhi, ikiwamo saratani kutokana na kukithiri kwa taka za plastiki zisizorejelezwa.
Hatari hiyo haiko kwa binadamu pekee. Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameonya kuwa mifugo nayo inaangamizwa na taka hizo; wanapomfanyia ng'ombe upasuaji, wanatoa tumboni kilo nne hadi tano za taka za plastiki.
Ni baa lililobainika katika Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), mahali hapo ni umbali wa Km 259 mashariki mwa Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Hii ni manispaa yenye jumla ya wakazi 471,409. Kati yao, wanawake ni 244,592 na wanaume ni 226,817 (Sensa ya Watu na Makazi, 2022). Wataalamu wa afya na mazingira wanatoa hadhari kuwa idadi hii ya wakazi na majirani zao, wako hatarini kukumbwa na maradhi kama vile saratani, kuhara, homa ya matumbo na maradhi ya mfumo wa upumuaji kutokana na kukithiri kwa taka za plastiki zisizokusanywa na kurejelezwa katika manispaa hiyo.
Kaimu Mkuu wa Kitendo cha Udhibiti Taka Manispaa ya Morogoro, Hezron Ligala anabainisha kuwa kati ya tani 377 za taka zinazozalishwa kila siku ndani ya manispaa hii, asilimia saba hadi 10 ni taka za plastiki. Hii ina maana kwamba tani 26.39 hadi 37.7 za taka za plastiki huzalishwa kila siku katika manispaa hii.
Hata hivyo, Ligala anasema ni asilimia nane tu ya taka zinazozalishwa katika manispaa, ndizo hukusanywa na kurejelezwa. Hivyo, tani 247 za taka hubaki mitaani kila siku na kuwaweka hatarini kiafya wananchi na mifugo dhidi ya taka hizo.
Katika uchunguzi wake, mwandishi wa habari hii amebaini kuwapo mrundikano wa taka za plastiki katika maeneo mbalimbali ya manispaa hii. Hayo ni pamoja na sokoni Mawenzi, Soko la Chifu Kingaru, Sabasaba na stendi ya daladala Mafiga iliyoko nje kidogo mwa mji wa Morogoro.
Mwandishi pia amebaini taka za plastiki zinatupwa katika Mto Morogoro unaoanzia maeneo jirani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo. Mto huo hupeleka maji Mto Ngerengere ambao ni sehemu ya vyanzo vikuu vya maji ya Mto Ruvu unaotegemewa na wakazi wa Pwani na Dar es Salaam kupata maji.
Kukiwa na ushuhuda huo, Kaimu Mkuu wa Udhibiti Taka, Ligala, anataja maeneo yanayozalisha taka za plastiki kwa wingi katika manispaa hii yanajumuisha masoko, maeneo ya biashara ya vyakula, vinywaji na kumbi za starehe.
Kuepuka madhara yatokanayo na taka hizo, Ligala anasema uongozi wa Manispaa ya Morogoro umekuwa unachukua hatua mbalimbali kudhibiti uzalishaji taka za plastiki.
Hatua hizo, Ligala anasema zinajumuisha kusimamia utekelezaji Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Sheria Ndogo za Afya na Mazingira za Manispaa ya Morogoro.
Katika hili la usimamizi wa sheria, Ligala anafafanua: "Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 (kifungu cha 4(1)) inatuelekeza tusimamie haki ya kila mtu anayeishi Tanzania kuwa katika mazingira safi na salama kiafya.
"Hivyo, kitendo cha kuwapo mrundikano wa taka, zikiwamo hizi za plastiki, ni ukiukwaji sheria unaohatarisha mazingira na maisha ya watu," Ligala anasema.
Anakiri tatizo la mrundikano wa taka za plastiki katika manispaa yao ni kubwa, akieleza kuwa dosari hiyo imekuwa mtihani mgumu kwao kuitatua kutokana na uwezo mdogo wa manispaa kukusanya taka na kuzirejeleza.
"Tunawashukuru watu ambao wameamua kujiajiri kwa kukusanya chupa za plastiki mitaani. Tatizo la taka katika manispaa hii mara kadhaa limekuwa linalalamikiwa na wananchi. Hii inatokana na wazabuni waliopewa jukumu la kuzoa taka mitaani kuacha kazi.
"Wazabuni wanatukimbia kutokana na ada ndogo ya taka inayokusanywa kila mwezi kutoka kwa wananchi," anasema Ligala na kufafanua kuwa awali manispaa ilikuwa inakusanya Sh. 1,000 kwa kila kaya kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Manispaa ya Morogoro ina kaya 133,809 zenye wastani wa wakazi watatu hadi wanne kwa kaya. Hii ina maana kwamba, kila mwezi manispaa inaweza kukusanya Sh. milioni 133.809 kutoka kwa wananchi kama tozo ya taka ikiwa kila kaya italipa Sh. 1,000.
"Kutokana na hali hii, manispaa imeamua kutunga Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2024 iliyoanza kutumika hivi karibuni baada ya kuona kuwa sheria iliyokuwapo awali haikidhi mahitaji na hivyo kuhatarisha maisha ya watu na viumbe hai wengine.
"Tulikuwa na sheria ndogo ya mwaka 2005 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010 na 2019, lakini baadaye mwaka huu imeonekana kutokidhi mahitaji ya sasa. Awali kila kaya ilikuwa inatakiwa kulipa Sh. 1,000 kwa mwezi kwa ajili ya taka, lakini fedha hizo zilionekana kutomudu gharama za uondoshaji taka katika manispaa.
"Wazabuni walitukimbia na kusababisha mrundikano wa taka kwenye maeneo mengi mitaani. Ninaamini sheria mpya ya mwaka 2024 itatusaidia kuweka mazingira yetu salama. Sasa kila kaya inatakiwa kutoa Sh. 3,000 kila mwezi kwa ajili ya uondoshaji taka," Ligala anasema.
Hata hivyo, Ligala anafafanua kuwa wakati ada ya taka ikiwa Sh. 1,000 kwa kila kaya, manispaa ilikusanya wastani wa Sh. milioni 40 kwa mwezi, na sasa wanakusanya wastani wa Sh. milioni 100 kwa mwezi.
Ni hali inayoonesha kutokuwapo ufanisi katika ukusanyaji mapato katika manispaa hii. Kwa kaya 133,809 zilizopo (Sensa 2022), manispaa ilipaswa kukusanya Sh. milioni 133.809 kwa mwezi kipindi ambacho tozo za taka zilikuwa Sh. 1,000 kwa kaya na sasa inapaswa kukusanya Sh. milioni 401.427 kwa mwezi kupitia tozo mpya za Sh. 3,000 kwa kila kaya.
Rashid Omary (47), mkazi wa Nanenane, Manispaa ya Morogoro, analalama kuwa licha ya ongezeko la tozo za taka, uondoshaji taka katika manispaa yao hauridhishi.
"Licha ya ongezeko la tozo kutoka Sh. 1,000 hadi 3,000 kwa kaya linalotuumiza wananchi, hasa tulio na kipato cha chini, bado taka hazizolewi kwa wakati na hivyo kuwapo mrundikano wa taka mitaani," Omary analalama.
MADHARA YA TAKA
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Clement Lubeya anasema mrundikano wa taka, mbali na kuchafua mazingira, pia huzalisha hewa mbaya ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Dk. Lubeya anasema mrundikano wa taka husababisha uozo unaozalisha na kuvutia wadudu wanaoeneza magonjwa mbalimbali ambayo ni hatari kwa binadamu, yakiwamo ya mlipuko, fangasi na minyoo.
"Uchafuzi wa mazingira ni hatari kwa afya ya binadamu. Kwa kawaida mwili wa binadamu hutoa hewa chafu na kuvuta hewa safi, hivyo kitendo cha kuishi au kupita eneo lenye mrundikano wa taka ni hatarishi kwake kwa kuwa huvuta hewa mbaya ambayo huathiri mfumo wa upumuaji," Dk. Lubeya anafafanua.
Bingwa huyo anasema taka za plastiki ni hatari zaidi kwa kuwa haziozi haraka, akitolea mfano chupa za maji ambazo kuzagaa kwake mitaani kunaweza kusababisha mitaro ya maji kuziba na hivyo kusababisha mafuriko.
"Chupa cha plastiki zikiziba mitaro, maji hupoteza mwelekeo wake na hivyo kuingia mitaani na kwenye makazi ya watu. Hicho kinakuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko, ikiwamo typhoid (homa ya matumbo) na kuhara.
"Chupa za plastiki kuna wakati huziba miundombinu ya maji taka na kusababisha kero kwa wananchi. Hii ni hatari kwa binadamu kwani ni rahisi jamii kuathirika kwa magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu," Dk. Lubeya anafafanua.
Bingwa huyo ana angalizo lingine, akieleza kuwa amebaini uzoaji taka mjini Morogoro haufuati kanuni za usalama kiafya; ameshuhudia baadhi ya magari yanayotukumika kukusanya na kubeba taka mitaani, yanaangusha taka hizo mitaani, hasa barabarani na hivyo kufanya taka za plastiki kuingia mitaroni, hata kuifikia mito mikubwa.
WATAALAMU SUA
Daktari wa Mifugo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Esron Karimuribo anasema madhara ya taka za plastiki hayaishii kwa binadamu pekee bali pia huathiri mifugo inayokula taka hizo.
Prof. Karimuribo anasema taka zote za plastiki huathiri mifugo, akiwatolea mfano ng’ombe na mbuzi ambao hula na plastiki zinazochanganyika na majani au nyasi.
"Taka hizi za plastiki zikiliwa na mifugo, huziba mfumo wa kumeng'enya chakula na kuleta changamoto ya kiafya kwa mifugo husika. Taka hizi pia husababisha vimelea vya magonjwa na kuathiri mifugo na wakati mwingine husababisha vifo kwa mifugo husika," Karimuribo anafafanua.
Mtaalam huyo anasema SUA ina hospitali yake kwa ajili ya utafiti wa mifugo, akiwa na ushuhuda wa kinachojiri hospitalini huko kwamba: "Pale mfugo (ng'ombe) upofanyiwa upasuaji, hukutwa tumboni mna kilogramu nne hadi tano za taka za plastiki. Kwa mfugaji asiye na uwezo wa kutibu mifugo yake, mifugo hiyo hufa kutokana na kula au kumeza plastiki."
KAULI YA NEMC
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro-Rufiji, Abel Sembeka anasema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 inakataza uchafuzi wa mazingira wa aina yoyote.
Anasema kifungu cha 118(1) cha sheria hiyo kinaelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga vituo vya kuweka taka kwa muda ambavyo vitatumika kukusanyia taka ngumu kwenye majiji, manispaa, miji au maeneo mengine ambayo kiwango kikubwa cha taka ngumu huzalishwa.
Sembeka anasema sheria inaelekeza jukumu la kusimamia taka ni la miji, halmashauri na manispaa kwa kuwa ndiyo wenye maeneo zinakozalishwa taka hizo, pia wanawatambua watu wao vizuri.
"Kazi yetu (NEMC) kwenye hili la taka, pale tunapoona kuwa kuna shida na wananchi wanalalamika, huwa tunaiandikia barua halmashauri husika ili ichukue hatua haraka za kuweka mazingira kwenye hali ya usalama ili kuepuka athari," anasema.
Sembeka anakiri kuwa na taarifa za tatizo la mrundikano wa taka za plastiki katika Manispaa ya Morogoro, akilitaja ndiyo sababu ya manispaa hiyo kushika nafasi ya mwisho kitaifa kwa miaka ya hivi karibuni kwenye utunzaji mazingira.
Manispaa ya Morogoro si eneo pekee linalokabiliwa na kukithiri kwa taka za plastiki. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) ya mwaka 2022 inaonesha zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka kote duniani.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati yake, chini ya asilimia 10 huchakatwa ili kutumika tena, huku kila mwaka zaidi ya tani milioni 19 hadi milioni 23 za plastiki huingia katika mito, maziwa na bahari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED