SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeagizwa kuendeleza kununua boti na vifaa vya kisasa vya uokoaji ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi majini kwa usalama.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, jijini Mwanza wakati alipokagua ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria kinachojengwa na TASAC.
Prof. amesema pindi ajali za majini zinapotokea, shughuli za uokoaji zinachelewa kufanyika kwa wakati kwa sababu ya kukosekana vifaa vya kisasa vya uokozi.
"Tunahitaji Watanzania katika maeneo ya maziwa na hata Bahari ya Hindi wafanye shughuli zao kwa usalama zaidi, hivyo vifaa vya kisasa vya uokoaji ni muhimu," amesema Waziri.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Hamid Mbegu, amesema tayari shirika hilo limeanza kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.
"Na katika mwaka ujao wa fedha tumepanga kununua boti tatu za uokoaji ambapo jumla tutakuwa na boti tano, tumezingatia viwango vya kisasa," Mbegu ameeleza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED