RC Macha apongeza mahakama kusikiliza mashauri kwa wakati

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 09:13 PM Jan 25 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amezindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga na kuipongeza Mahakama kwa ufanisi wake katika kusikiliza mashauri kwa wakati na kutoa haki kwa wananchi.

Macha amezindua maadhimisho hayo leo, Januari 25, 2025, katika viwanja vya Zimamoto, vilivyopo eneo la Nguzonane, Manispaa ya Shinyanga. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Macha amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya sheria, kujua kazi za Mahakama, na namna ya kufungua mashauri ili waweze kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

“Maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria ni muhimu sana kwa wananchi, kwani kuna watu wengi wanashindwa kupata haki zao kutokana na kutokujua sheria. Hivyo, ni vyema wakajitokeza kwa wingi kwenye vibanda na wapate elimu ya sheria, namna ya kufungua mashauri mahakamani, pamoja na kujua kazi za Mawakili,” amesema Macha.

Pia, Macha ameipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kwa kasi kubwa ya kusikiliza mashauri.

 Amesema kuwa mwaka jana (2024) hakuna viporo vya mashauri na kwamba mashauri yote yalikuwa yamesikilizwa kwa wakati.

 Ameisihi Mahakama iendelee na kasi hiyo ya ufanisi mwaka huu (2025).

Katika hatua nyingine, Macha amezungumzia Mahakama za Mwanzo na kusema kuwa kuna haja ya kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri katika ngazi hizo ili wananchi waweze kupata haki zao kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Macha, pia amewataka wananchi kutii maamuzi ya Mahakama na kwamba ikiwa hawajaridhika na maamuzi hayo, wanapaswa kukata rufaa na kwenda ngazi za juu zaidi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali, ameeleza kuwa katika Wiki ya Sheria, elimu ya sheria itatolewa bure kwa wananchi kupitia vibanda mbalimbali vilivyopo viwanja vya Zimamoto na maeneo ya mikusanyiko, magereza, mashuleni na vyuo.

Amesema maadhimisho hayo yatanogeshwa na bonanza la michezo mbalimbali, ambalo litafanyika jijini Mwanza tarehe 1 Februari, huku kilele cha Wiki ya Sheria kikifanyika tarehe 3 Februari katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.

Aidha, maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria yanaashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka mpya, baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama, ambayo huanza tarehe 15 Desemba na kumalizika tarehe 31 Januari kila mwaka.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka huu inasema: “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”