JK aonya wanaotumia dini kujenga chuki

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 08:30 AM Jan 25 2025

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk.Jakaya Kikwete.
Picha:Mtandao
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk.Jakaya Kikwete.

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk.Jakaya Kikwete amewaonya Watanzania kuacha kutumia mwamvuli wa dini kujenga chuki na kuleta mifarakano katika jamii hali inayochochea machafuko na uvunjifu wa amani.

Kikwete ambaye ni mwasisi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), alisema hayo mjini Morogoro  wakati wa kikao cha kamati ambapo akawaasa viongozi wa dini kusimama imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa  kisiwa cha  amani, utulivu na umoja.

Alisema amani na utulivu kamwe haviwezi kununuliwa dukani badala yake ni lazima Watanzania waendelee kuimarisha undugu na mshikamano na kuepuka kubaguana kwa misingi yoyote ikiwamo ya kiimani, rangi wala kabila.

 Alitolea mfano chachu ya kushauri uanzishaji wa taasisi hiyo enzi za serikali aliyoiongoza kuwa kulisababishwa na mgogoro wa kidini ulioibuka wa kuchinja, kati ya waumini wa kiislam na kikristo ambapo licha ya kuanzia eneo dogo la Katoro, watu waliusambaza na kuuchochea kuwa wa kiimani na kuleta machafuko, mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali.

 "Hali ilikuwa mbaya, kila mmoja akachukua upande wake, ikabidi tuanze kuwadhibiti watu na hata vyombo vya habari vilivyoonekana kuchochea mgogoro na ndio kama alivyosema Sheikh Alhad (Sheikh Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania) tukaitisha mkutano mkubwa sana kuwahi kutokea kwa kuwashirisha viongozi wa dini zote, wakala na kulala pamoja ili kila mmoja amzoee mwenzake na ikawa mwanzo wa kuanzisha chombo hiki," alisema Rais huyo Mstaafu.

 Mstaafu Kikwete akaielekeza taasisi hiyo kuendelea kusimamia, amani, maadili na utulivu na kusaidia utatuzi wa changamoto ya  migogoro ya wakulima na wafugaji na kukiri tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 migogoro hiyo imepungua.

Aidha, akataka waongeze nguvu ili vijana wa Tanzania waishi katika mila na desturi za Tanzania na kuondokana na changamoto ya uvunjifu wa amani, kwani bado kuna changamoto kwenye malezi hivyo wasimamie ili vijana wasiharibike na utandawazi.

 Akakemea baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumika kuchochea uvunjifu wa amani na kwamba havitavumilia hali hiyo. 

 Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema taasisi hiyo haina lengo la kufanya ibada za dini mseto na sio chombo cha dini kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

 Alisema kinachofanyika ni kuwaunganisha viongozi wa dini pamoja na kutafuta amani na utulivu wa nchi huku kila dini ikiendelea kuabudu kwa imani yake na kila mmoja anafahamu imani yake na kuiishi.

 Sheikh Alhad pia akawahimiza viongozi wa dini kufanya matendo mema kwani wao wanafananishwa na chumvi  ambayo ni kiungo muhimu  ambayo ikichafuka haiwezi kusafishwa na kitu chochote. 

 Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema mkoa wa Morogoro  miaka ya zamani ulikuwa ukisifika kwa migogoro ya ardhi na wakulima na wafugaji ambapo tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo sifa hiyo haipo tena.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini JMAT, Azim Dewji alisema jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja na hata vyama vya siasa ni yema vikalinda hili na kufanya siasa ya staha kwasababu Tanzania ni yetu sote.