Ujio kiongozi wa Libya kuongeza uwekezaji nchini

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:32 AM Jan 26 2025
Jiji la Dar es Salaam
Picha: Mtandao
Jiji la Dar es Salaam

RAIS wa Baraza la Urais la Libya, Mohamed Menfi, anatarajia kufanya ziara nchini akiongozana na ujumbe mahsusi na maofisa wa ngazi za juu katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati.

Mkutano huo ambao unahusu nishati unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari, mmoja wa wafanyabiashara katika sekta ya madini kutoka Libya waishio Tanzania, Mohamed Abubakar, alisema ujio wa Rais huyo na msafara wake, utafungua milango kwa wawekezaji wengi kutoka Libya.

Kwa mujibu wa Abubakar, ujio huo utaongeza fursa kwa Watanzania kuungana na wafanyabiashara wa Libya katika nyanja mbalimbali za uwekezaji.

Alisema miongoni mwa watakaoambatana katika msafara huo ni Waziri wa Fedha na Waziri wa Nishati wa nchi ya Libya. 

“Lengo likiwa kuingia makubaliano katika nyanja mbalimbali zikiwamo sekta za elimu, uchumi na biashara. Pia baadhi ya mikataba itatiwa saini katika ziara hii,” alisema.

Alisema katika sekta ya uchumi na biashara moja ya benki nchini Libya itaingia makubaliano ya kufungua tawi lake Tanzania.

Alisema Libya  inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kiimani (kidini) katika kuhakikisha wanasaidia taasisi za Kiislamu zinazotoa misaada ya kijamii na kusaidia vituo mbalimbali vya kulea watoto wenye mahitaji maalumu.

Machi, mwaka jana, Balozi wa Libya nchini, Abdelmajed Shetawia, alipopeleka hati za utambulisho kwa Rais Samia Suluhu Hassan, alizungumzia suala hilo.