WAKATI timu ya Mwembe Makumbi City ikishuka uwanjani leo kupepetana na Maafande wa JKU SC katika mchezo wa kiporo wa kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi kuu Zanzibar, itaanza kutumia nyota wake wapya, lakini pia ikicheza kwa tahadhari kubwa kutokana na ukosefu wa wapinzani wao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Rajab Mrisho, alisema anakutana na timu ambayo inauzoefu mkubwa katika mashindano ya nje na ndani, hivyo lazima aingie kwa tahadhari na heshima ili kufanikisha mpango wake.
Alisema mbali na uzoefu wa kimashindanao, lakini pia wana wachezaji wazuri wakuelewa mbinu za mchezo mapema.
Mrisho alisema ingawa wapinzani wao hawapo vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, hiyo haiwafanyi kubweteka katika michezo hii ambayo timu zote zimeimarisha vikosi vyao kupitia usajili wa dirisha dogo.
Alisema katika kuelekea mchezo huo timu yake itaendelea na mwenendo ule ule walioanza nao mwanzo wa msimu ili kuona wanachokihitaji wanakipata.
“Tunashuka uwanjani kuhakikisha hatupotezi malengo hasa kupata point tatu katika mchezo huu muhimu, tunaenda kupambana na najua si mchezo rahisi, lakini tutashinda,” alisema.
Aidha, alisema katika mchezo huo atakuwa na ingizo jipya la wachezaji ambao wamewasajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo.
Kocha huyo alisema kupitia wachezaji wake hao wapya na wale wa zamani, anaamini watafanya vizuri katika mchezo huo muhimu kabla ya kuanza michezo yao ya mzunguko wa lala salama.
Mwembe Makumbi City inashuka uwanjani ikiwa nafasi ya tatu na alama zake 27, wakati wapinzani wao JKU SC wakiwa nafasi ya tisa na alama zao 21.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED