Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita imewataka wanawake wajawazito kufika mapema katika vituo vya afya mara wanapogundua kuwa ni wajawazito ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kulea ujauzito kwa usalama na kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kujifungua.
Mganga mfawidi wa hospitali ya Mkoa wa Geita ambae pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake hospitalini hapo Mfaume Kibwana ametoa ushauri huo wakati taasisi ya Wanawake na Samia walipotembela hospitali hiyo na kutoa zawadi mbalimbali kwa wanawake waliojifungua ikiwa ni sehemu ya kusherekea siku ya kuzaliwa ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Kibwana amesema changamoto za uzazi zimeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za wajawazito na watoto wao.
"Tunakutana na visa vingi vya wanawake wenye matatizo kama upungufu wa damu, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, na kifafa cha mimba, ambayo kwa kiasi kikubwa yanazuilika iwapo wajawazito watahudhuria kliniki na kupata huduma zinazotakiwa mapema," amesema Kibwana.
Kibwana amesema baadhi ya matatizo yanayo2wakumba kina mama wanaoletwa hospitalini hapo kwa huduma za kibingwa zinatokana na wengi kuchelewa kuhudhuria kliniki, huku wengine wakijifungulia majumbani bila usimamizi wa kitaalamu.
"Ni muhimu wajawazito kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kupata chanjo muhimu, kufuatilia maendeleo ya mimba na kujua hatari zozote zilizopo hii itasaidia kujua hatari na namna gani ya kukabiliana nayo," ameongeza Dk Kibwana.
Aidha amewashauri wajawazito kuzingatia lishe bora, kuepuka kazi ngumu, na kuzingatia ushauri wa madaktari ili kuhakikisha ujauzito unakuwa salama na kujifungua kwa mafanikio.
Akizungumzia hali ya hospital hiyo Dk Kibwana amesema kwa sasa wameimarisha huduma zake kwa kuongeza idadi ya wataalamu wa afya, vifaa tiba, na elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa huduma za afya ya uzazi.
Kaimu Mwenyekiti Wanawake na Samia Mkoa wa Geita Mariam Sharifu amesema katika kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa Rais Samia wao kama wanawake wameguswa kufika hospitalini hapo kufanya matendo ya huruma yaliyoambatana na ugawaji wa vitu na kupanda miti.
Amesema wanawake wanatambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia ya kuwaletea wananchi maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED