ABIRIA na watumiaji wa vyombo vya moto katika eneo la kivuko cha Kigongo-Busisi, mkoani Mwanza wamelazimika kuvunja geti na kupita daraja la dharura linakojengwa daraja kubwa la J.P Magufuli baada ya vivuko kusitisha huduma kwa zaidi ya saa sita.
Kadhia hiyo ilitokea juzi na kusababisha wasafiri wanaokwenda maeneo mbalimbali kukaa kwa muda mrefu wakisubiri huduma hiyo na kulazimu kuvunja na kupita katika daraja hilo.
Akizungumzia adha hiyo kwa niaba ya wasafiri wenzake, John Kipingwa, alisema wamekaa katika kivuko kwa saa tano huku akiiomba serikali kuharakisha jitihada za kumaliza ujenzi wa Daraja la J.P. Magufuli.
Alisema tatizo hilo limekuwa kubwa na la muda mrefu kutokana na wakati mwingine kinabaki kivuko kimoja ambacho hakiwezi kumudu usafirishaji katika eneo hilo lenye shughuli kubwa za usafiri na usafirishaji.
Majid Bashiri, alisema amekuwa katika kivuko hicho kwa zaidi ya saa sita huku akishangazwa na vyombo vyote vya usafiri kuharibika kwa mkupuo jambo linaloleta shida kwa abiria na watumiaji wa vivuko hivyo.
Aidha, alisema baada ya kuuliza waliambiwa kuwa vivuko vyote vimeharibika kutokana na kuingiliwa na magugu maji katika masanduku ya kupozea injini ambayo yalisababisha injini kutofanya kazi kwa ufanisi.
“Tumekaa hapa kwa muda mrefu na mara kadhaa suala hili limekuwa likijirudia, lakini tumeomba kufunguliwa kwa dharura kupita katika daraja la dharura hatujasikilizwa hivyo kulazimika kuvunja na kuvuka kwa mguu kuelekea upande wa pili,” alisema Bashiri.
Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa, Mhandisi Vitalisi Bilauli, alisema tatizo lililojitokeza lilisababishwa na magugu maji ambayo huingia katika masanduku ya kupozea injini.
Alisema hatua hiyo inasababisha kuongezeka kwa joto ambalo halitakiwi na kushambulia injini za vivuko hali inayosababisha kutofanya kazi kwa ufasaha.
“Hadi sasa mafundi wanaendelea na jitihada ili kuhakikisha wanaondoa tatizo hilo ikiwemo kusafisha injini za Vivuko vyote. Mpaka sasa kivuko cha MV. Misungwi tayari kimesafishwa na kinaendelea na usafirishaji hivyo tunaomba wananchi kuwa watulivu,” alisema Bilauli.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, alikiri kutokea kwa kadhia ya usafiri wa vivuko vyote vinavyofanywa safari zake kati ya Kigongo-Busisi.
Elikana alisema chanzo cha kukwama kwa vivuko hivyo ni kuibuka kwa wimbi la magugu maji ambayo yalizuia shughuli hizo kutokana na usalama katika usafirishaji.
"Kwa sasa kwenye suala la mazingira tuna hii kero kubwa ya magugu maji yamekuwa yakizuia shughuli za kiuchumi majini kama tunavyojua Mkoa wetu sehemu kubwa imezungukwa na Maji hivyo magugu haya yanazuia shughuli za kiuchumi ikiwamo pia uvuvi," alisema Balandya.
Aidha, aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya mazingira mkoani hapa kuhakikisha yanawekeza katika utafiti kudhibiti hali hiyo.
"Kama serikali tupo tayari kuunga mkono kwa namna yoyote wadau wetu watakao jitokeza kupata mwarobaini wa magugu hayo,"alisema Elikana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED