Zahanati ya millioni 241 yawanufaisha wananchi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 08:38 PM Jan 29 2025
Zahanati  ya million 241 yawanufaisha wananchi.
Picha: Neema Emmanuel
Zahanati ya million 241 yawanufaisha wananchi.

WANANCHI wa kata ya Mihami wilayani Ilemela wamenufaika na ujenzi wa zahanati wa shilingi million 241 uliotekelezwa na TASAF kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali maendeleo.

Paskazia Sabwoya ni  Mtendaji wa Mtaa wa Mihana, hapa anaeleza kuwa mradi huo umesaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hivyo kuzuia vifo vya akinamama wakati wa kujifungua, upatikanaji wa chanjo, huduma ya afya ya uzazi, maendeleo ya mtoto na lishe na uboreshaji wa afya ya jamii.

“Mradi huu umegharimu shilingi milioni 241 ambapo TASAF imetoa 225 nyingine imetoka kwa jamii" anaeleza.

Naye Agness Levocatus mkazi wa mtaa wa Mihama anaeleza kuwa Mradi huo ni muhimu  kwao kwa sababu walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

“Tulikuwa tunaenda mpaka kirumba na ukifika huko wanakuambia uende Sekou-Toure, tulikuwa tunahangaika sana, kuna wengine walikuwa wanajifungulia njiani, wanapoteza maisha mama na mtoto, na tumepoteza ndugu zetu wengi sana kwa muda mrefu kwa sasa, tunafurahia kituo hiki cha afya kuwa katika eneo letu” anaeleza.

Aidha Leonard Robert, Mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela anaeleza kuwa tangu mwaka 2020 hadi Desemba mwaka jana jumla ya walengwa 3450 wamenufaika na ruzuku ya zaidi ya Billion 6.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo kutoka mwaka 2021 hadi Desemba mwaka jana jumla ya miradi 46 yenye thamani ya zaidi ya billion 2.2 imeshapokelewa kwenye Manispaa hiyo kwa ajili ya kutekelezwa, miradi hiyo ni kati ya jumla ya miradi 33 ambayo imeshakamilika, huku 13 ikiwa bado inaendelea na utekelezwaji.