KUZALIWA mtoto, ni tukio la kipekee linaloleta furaha kubwa katika familia. Hata hivyo, hali inakuwa ngumu mtoto huyo anapozaliwa na matatizo kiafya, kama vile kuwa njiti (kazaliwa kabla ya muda wake wa kawaida).
Wazazi wa watoto njiti hukutana na changamoto kubwa hasa katika mazingira ya kazi, hasa katika taasisi za umma, kutokana na sera za kazi ambazo mara nyingi hazilengi mahitaji maalum ya wazazi hao.
Katika sehemu za kazi nyingi za umma na binafsi, mazingira hayazingatii changamoto wanazokutana nazo wazazi wa watoto njiti.
Baadhi ya changamoto hizo, ni ukosefu wa maeneo maalum kwa ajili ya kunyonyesha, kupumzika au kutoa maziwa ya akiba.
Wazazi wanachohitaji ni muda wa ziada kuwahudumia watoto njiti na mara nyingi hukutana na vikwazo, kwani taasisi nyingi hazina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo.
Ni hali inayowafanya wazazi wahisi ama kutengwa au kudharauliwa, pale wanapohitaji kushughulikia mahitaji ya mtoto wao.
Mnamo Mei Mosi mwaka jana, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango akatoa neno katika hilo likieleza ikiwa mfanyakazi atajifungua mtoto njiti, kipindi cha uangalizi maalum hakiwezi kuhesabiwa kama likizo ya uzazi.
Likizo ya uzazi huanza tu baada ya mtoto kumaliza kipindi cha uangalizi maalum, kulingana na tathmini ya madaktari.
Aidha, anasema mfanyakazi ataruhusiwa kutoka kazini kwa muda wa miezi sita baada ya likizo ya uzazi, ili kumwezesha kwenda kunyonyesha mtoto wake.
Dk. Mpango anasisitiza suala la afya ya mama na mtoto na hususan njiti ni kipaumbele kwa serikali ya Awamu ya Sita, ambayo kisheria kunatafsiriwa kuwapo likizo ya uzazi kwa wanawake wanaojifungua watoto kwa muda wa siku 84 ikiwa ni mtoto mmoja au siku 100 ikiwa ni zaidi ya mmoja.
Kiuhalisia, watoto njiti wanatajwa kuhitaji uangalizi wa karibu na kila mara, kwa sababu ya afya yao dhaifu, jambo linalowafanya wazazi kuwa na mahitaji maalum ya muda wa ziada au ruhusa za mara kwa mara.
Inatajwa mara nyingi waajiri hawaelewi hali hii inayosababisha wazazi kuhisi shinikizo la kutosheleza matarajio ya kazi huku wakihangaika na majukumu ya kifamilia.
Ofisi za umma katika mustakabali wa ustawi wa jamii kazini, nazo zaelezwa kuhitaji kuwa na maeneo maalum kwa ajili ya wazazi kunyonyesha au kupumzika, huku huduma za msaada wa kisaikolojia zikihitajika kwa wazazi wa watoto njiti.
Hiyo ni pamoja na kuimarisha miongozo ya kisheria, huku serikali ikiingiza vipengele vya ulinzi kwa wazazi wa watoto njiti katika sheria za ajira na sera za afya ili kuhakikisha haki zao zinazingatiwa kikamilifu.
WHO NA ILO
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kazi Duniani (ILO), pia zina miongozo inayolenga kulinda afya ya mama na mtoto, pamoja na haki za wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti.
Sera na Miongozo ya WHO na ILO
WHO, zinasisitiza umuhimu wa huduma bora kwa mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na uangalizi maalum kwa watoto njiti.
Shirika hilo tayari lina miongozo inayopendekeza utoaji huduma za afya zinazozingatia mahitaji maalum ya watoto njiti na msaada kwa wazazi wao.
Kwa upande wake ILO, kuna Mkataba wa Ulinzi wa Uzazi (C183) wa mwaka 2000, unaopendekeza likizo ya uzazi ya angalau wiki 14 kwa wanawake wanaojifungua, pamoja na ulinzi wa ajira na haki za wafanyakazi wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
Ingawa mkataba huo hauzungumzi moja kwa moja kuhusu watoto njiti, unatoa msingi wa sera za kitaifa zinazoweza kuzingatia hali maalum kama hizi.
Inatajwa kwamba utekelezaji wake katika nchi wanachama wa WHO na ILO, zinahimizwa kuendeleza sera na sheria zinazolinda haki za wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti.
SURA YA TANZANIA
Nchini Tanzania serikali imetangaza kuwa kipindi cha uangalizi maalum kwa watoto njiti hakitahesabiwa kama sehemu ya likizo ya uzazi na likizo hiyo itaanza tu pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum, kama itathibitishwa na madaktari.
Serikali pia inaendelea kuwekeza katika huduma za kihospitali kama vile ujenzi wa wodi maalum za uangalizi wa watoto njiti na kupeleka vifaa vya kusaidia watoto hata katika vituo vya kutoa huduma za afya, ikiwamo mashine za kusaidia kupumua.
ELIMU NA UHAMASISHAJI
Katika eneo kila tarehe 17 ya Novemba, kila mwaka, Tanzania huadhimisha Siku ya Watoto Njiti Duniani, kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wake, pia kuwajali watoto njiti na kuhakikisha wanapata haki zao.
Pia, Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), inalenga kuhakikisha watoto wanapata malezi bora kuanzia utotoni, ikiwa ni pamoja na watoto njiti.
Dorice Mollel, Mkurugenzi wa asasi ya Dorice Mollel Foundation anasema: “Watoto njiti wanahitaji uangalizi wa kipekee na wazazi wao wanapaswa kuungwa mkono kwa kila hali.“Kama jamii na waajiri, tunapaswa kuzingatia kwamba wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti wanahitaji si tu muda wa ziada kwa ajili ya kujali watoto wao, pia wanahitaji msaada wa kisaikolojia na huduma za afya zinazozingatia mahitaji maalum ya familia zao."
Anashauri kuwapo taasisi za umma na serikali zinazopaswa kuboresha sera, zitakazohakikisha kunakuwapo haki za wazazi kama vile kutoa likizo ya ziada kwa ajili ya uangalizi maalum wa mtoto na kuzingatia mazingira bora kazini.
Dorice anazitaja hizo zitawasaidia wafanyakazi kuwajibika kazini kwao kwa ufanisi, pasipo kuwa na shinikizo la kupuuza majukumu ya kifamilia yanayowakabili.
"Katika Dorice Mollel Foundation, tunaamini kuwa ulinzi wa haki za wafanyakazi, hasa wanawake wanaojifungua watoto njiti, ni sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii.
“Kwa hiyo, tunaunga mkono juhudi zote zinazolenga kuboresha sera na huduma kwa wazazi wa watoto njiti." anasema Dorice, akiwa na maelezo ya ziada kuwa:
"Tunatambua changamoto kubwa wanazokutana nazo wazazi wa watoto njiti, hasa wanawake wafanyakazi.
“Ni muhimu kwamba wapewe muda wa kutosha na mazingira bora ya kufanya kazi, ili waweze kumhudumia mtoto wao na kujihusisha na majukumu ya kifamilia kwa usawa.”
Kinachopendekezwa sasa kitaalamu ni kwamba, waajiri waweke sera zinazohusiana na uangalizi wa watoto njiti, ikiwamo kutoa maeneo maalum kwa ajili ya kunyonyesha na kupumzika.
Pia, kunatajwa haja ya kuwapo msaada wa kisaikolojia, ili kuwasaidia wafanyakazi watekeleze majukumu yao ya kifamilia.
Hicho ndicho kinachoifanya serikali, pia waajiri kuhitaji mabadiliko yanayohakikisha kuwa haki za wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti zinazingatiwa kikamilifu na kwa kufanya hivyo, tutakuwa na jamii yenye wafanyakazi wenye afya bora na familia imara.
SAMIA NA NJITI
Hulka ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inajionyesha katika tukio la Julai mwaka juzi alipotoa shilingi milioni mbili kwa Mariam Mwakabungu (25), aliyejitolea kukumbatia watoto njiti katika Hospitali ya Rufani Mkoa Amana, jijini Dar es Salaam. Mganga Mfawidhi wa Amana Dk. Bryson Kiwelu, akasema kuwa umma umeguswa na anachokifanya Mariam, akiwamo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuweka kipaumbele kwenye uboreshaji huduma za afya uzazi, mama na mtoto.
"Rais ametoa shilingi milioni mbili fedha taslimu kumpatia mama huyu, kwa kujitoa kwake na amewapongeza viongozi wa Wizara ya Afya na Amana kwa ubunifu huu na uthubutu wa mama huyu kuwa sehemu yetu,” akatamka Dk. Kiwelu.
Ni hali iliyomtia hamasa kwa kuungawa mkono na Rais katika tendo hilo, hospitalini Amana, Mariam akieleza: “Sikutegemea nimeona kama ndoto Mimi nilikuwa najitolea tu nimeona kama jambo dogo kwangu niliona tu kama jambo la kawaida sikujua kama litafikia huku."
Hapo, mdau anayewaunga mkono watoto njiti, Mkurugenzi wa taasisi ya Dorice Mollel, akakisifu kitendo alichokifanya Mariam ni cha utu na ametoa mchango mkubwa kuokoa maisha ya watoto hao.
“Nampongeza sana Mariam, bado ni mdogo angeweza kufanya shughuli nyingine, lakini ameguswa kusaidia watoto hao njiti,” anatamka Dorice.
Pia, Oktoba mwaka jana, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufani ya Amana, zikaandaa harambee kuchangia ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajawazito, fedha zinazopatikana kutumika kununua vifaa tiba.
Hafla hiyo ya uchangiaji iliyofanyika Oktoba 25, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, shilingi Bilioni 1.2 zilikusanywa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, akamuwakilisha Rais Dk. Samia.
Ndio kauli kama hiyo ya mwaka ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, anayesema “Rais.Dk. Samia kaokoa maisha ya watoto njiti, kwa kuongeza Wodi ya Mama na Mtoto kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bahi”
Hiyo inaungana na kauli ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, mwaka jana aliyetamka, kila mwaka nchini kuna watoto 200,000 wanaozaliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED