Utaalamu mpya; Mate kubaini mwenye kisukari

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:36 PM Jan 30 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi
Picha: MNH
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi

MKURUGEZNI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema hospitali hiyo, inatarajia kuja na kifaa cha kisasa cha kupima ugonjwa wa kisukari kwa njia ya mate.

Amesema kutokana na kukua kwa matumzi ya vifaatiba vya kiteknolojia duniani, hospitali hiyo yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa ni matarajio kuwa na aina tofauti za utaalamu wa hali ya juu na kisasa.

Prof. Janabi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, muda mfupi baada ya MNH kukabidhiwa vifaatiba mbalimbali, vyenye thamani ya Sh. milioni 125, ikiwamo maalumu kwa ajili ya kukuza uoni wa mishipa ya damu na fahamu wakati wa upasuaji.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, kwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, hospitalini hapo, kwa niaba ya Serikali ya Watu wa China, jijini Dar es Salaam.

“Tutakapokuwa tayari tututaarifu umma kupitia nyinyi waandishi wa hbari. Tutakuwa na kifaa kipya cha kupima kisukari kwa njia ya mate,” alisema Prof. Janabi.

Kisukari hupimwa kwa njia mbili; damu na mkojo. Utaalamu mpya kuongeza ufanisi. (Mtandao)
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa sugu ambao mtu yeyote anaweza kuugua.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 422 wanaishi na ugonjwa wa kisukari duniani kote, ikiwa ni mara nne zaidi ya miaka 40 iliyopita, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ugonjwa wa kisukari hutokea wakati mwili hauwezi kutumia sukari inayotengenezwa na mwili (glucose) yote katika damu.

Kwa kawaida glucose yenyewe si mbaya, kwani nimafuta ya seli zote katika mwili kwa baadhi ya tishu, kutumia glucose hiyo, zinahitaji hatua ya insulini, ambazo ni homoni zinazozalishwa na kongosho ambayo inaruhusu sukari hiyo kupenya kwa urahisi zaidi ndani ya seli na hivyo kubadilishwa kuwa nishati.

Matatizo ya kisukari yanaweza kusababisha mshtuko wa moyo, kiharusi, upofu, kushindwa kufanya kazi kwa figo na kukatwa kwa viungo vya mwili.

Licha ya hatari, watu wengi wenye ugonjwa wa kisukari hawajui kuwa wanao. Mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kuzuia mtu kuugua kisukari.