Mwimbaji mkongwe wa muziki wa taarab, Khadija Omar Kopa, pamoja na msanii wa kizazi kipya, Barnaba Classic, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka 65 ya kuzaliwa na kumtakia maisha mema.
Katika kipindi cha Sentro Bash kinachorushwa na Clouds TV, kila mmoja kwa wakati wake alitoa pongezi kwa Rais na kumwombea maisha marefu ili aendelee kuiongoza Tanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
"Rais Samia ni ndugu yangu, namuombea Mwenyezi Mungu amzidishie nguvu na ari ya kuliongoza taifa, pamoja na hekima zaidi katika kulitumikia," alisema Kopa.
Msanii huyo aliongeza kuwa Rais Samia alichukua uongozi katika kipindi kigumu, lakini sasa kila Mtanzania anashuhudia maendeleo katika nyanja mbalimbali.
"Kama wasanii na wanamichezo, tunathamini mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya michezo, ikiwemo soka kupitia kampeni ya ‘Goli la Mama,’ pamoja na mchezo wa masumbwi," aliongeza Kopa.
Kwa upande wake, Barnaba Classic alisema anamshukuru Rais kwa kuthamini sanaa na wasanii wa Tanzania, akifafanua kuwa yeye ni miongoni mwa waliopata fursa ya kutoa burudani katika hafla nyingi za kitaifa, ikiwemo zile zinazofanyika Ikulu.
"Sina budi kumtakia maisha mema na afya njema anapotimiza miaka 65, ili aendelee kuliongoza taifa kwa hekima," alisema Barnaba katika kipindi hicho.
Aidha, Barnaba aliishukuru Clouds TV kwa kuungana na Watanzania kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia kupitia kipindi hicho.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Christina Mndeme, alimtaja Rais kama kiongozi shupavu mwenye maono makubwa kwa taifa.
"Tunamuombea Mwenyezi Mungu ampe uhai na hekima zaidi ili aendelee kuiongoza Tanzania kwa mafanikio. Watanzania tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutupa kiongozi msikivu," alisema Christina.
Christina alikuwa miongoni mwa viongozi waliopiga simu moja kwa moja studio na kutoa salamu zao za pongezi kwa Rais Samia katika kipindi hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED