MADAI ya malimbikizo ya mishahara ya waandishi wa habari 10 dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe yametua mbele ya Jaji Dk. Modesta Opiyo, waandishi wanaomba akamatwe aende gerezani.
Wadai wamewasilisha maombi hayo na yamepangwa kusikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Wadai hao wamefikia hatua hiyo baada ya Dudley, mtoto wa Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kushidwa kulipa malimbikizo hayo.
Maregesi Paul na wenzake tisa, waliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kumkamata Dudley na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya mishahara yao baada ya kushinda tuzo.
Januari 14, mwaka huu, Dudley alionywa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio, wakati shauri hilo la madai lilipokuwa likitajwa na kuamuliwa kufika mahakamani na kulipa kabla ya Januari 31, 2025.
Wakili Samadani Mngumi, aliyemwakilisha Dudley, alidai alikuwa hajazungumza na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru.
Awali, Mahakama ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai, 2023.
Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17, mwaka 2023, mbele ya Msuluhishi wa CMA Ilala, Bonasia Mollel.
Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh. milioni 114 lakini baada ya kukaa mezani kwa majadiliano kwa pamoja, kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh. milioni 62.7.
Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30, mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari, mwaka jana, lakini hakulipa.
Hata hivyo Dudley aliingia makubaliano ya kulipa malimbikizo hayo nje ya Mahakama, Aprili hadi Mei, mwaka jana, lakini pia hajafanya hivyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED