Wakulima watilia shaka mizani inayopima pamba

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:10 PM Jan 30 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (kulia), akimkabidhi mkulima wa kijiji cha Manungu kata ya Uyogo, halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, Paul Mwazalima, bomba la kunyunyuzia dawa la kuua wadudu shambani, wakati wa ziara ya kukagua hali ya uza
Picha ; Shaban Njia
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (kulia), akimkabidhi mkulima wa kijiji cha Manungu kata ya Uyogo, halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, Paul Mwazalima, bomba la kunyunyuzia dawa la kuua wadudu shambani, wakati wa ziara ya kukagua hali ya uza

WAKULIMA wa zao la pamba katika halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, wameilalamikia mizani inayotumika kupima zao hilo, wakidai inawaingiza hasara.

Wanadai  kutofautiana kwa mizani na ile mikubwa inayotumika viwandani inaleta utata na kuwakatisha tamaa ya kuendelea kulima zao hilo.

Mkulima wa kijiji cha Manungu, kata ya Uyogo, halmashauri hiyo, Juma Athumani, alibainisha haya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.

Macha alikuwa katika ziara ya kukagua hali ya uzalishaji wa zao hilo, huku msimu huu Kahama ikitarajia kuzalisha zaidi ya kilo milioni 10.Alisema, wamekuwa wakipata hasara kila msimu kwa sababu ya mizani wanayoitumia sokoni vijijini, kutofautiana na ile ya viwandani na kuiomba serikali kuingilia kati na kutatua tatizo hilo.

“Tunawalalamikia wahasibu wetu kila masoko tukijua wao ndio wanatuingiza hasara, kumbe mizani yetu tunayotumia inatofautiana na ile ya viwandani hasa wakati wa kupima gari lililobeba pamba.

“Tunaomba serikali iangalie namna ya kulitatua hili ili tusikate tamaa ya kulima zao hili. Bodi ya pamba kwa isicheleweshe viuatilifu na bomba za kupulizia dawa shambani, inasababisha wadudu kushambulia mmea na kupata mavuno kidogo kulinganisha na ukubwa wa mashamba wanayoyalima,” aliongeza Athumani.

Andrew Iboliti, alisema viuatilifu na bomba zinazotumika kupulizia dawa shambani haziwafikii kwa wakati, hulazimika kuazima kwa wakulima wenzao walionazo vifaa hivyo, ingawa havikidhi mahitaji.

Shamba la pamba
Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kahama, Emmanuel Kileo, alikili kuwapo kwa malalamiko hayo na kunapotokea shida ya kupishana kwa mizani, wanasitisha ushushaji na kuanza kupima upya na kupata uwiano.

Kuhusu bomba alisema, bomba hizo ni gharama kubwa na zinapopatikana zinafikishwa katika vyama vyao vya msingi, isipokuwa wenye ekari tano na kuendelea hupewa moja kwa moja.

Alisema msimu huu tayari wamepokea bomba 1,500 na atahakikisha zote zinawafikia wakulima.

Macha aliiagiza bodi hiyo, kuhakikisha inawafikia wakulima, kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili, ili kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaongezeka na ni moja ya kazi aliyopewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Aliwataka maaofisa kila kijiji na kata, kuhakikisha wanawakumbusha wakulima kanuni 10 za kilimo hicho, ikiwa ni pamoja na kuwashauri namna ya kulima kisasa, kuondokana na kupata kilo 700 katika ekari 10 huku akiwasisitiza wakulima kuacha kuuza pamba kinyemela.