Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na nchi ya Burundi katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya nishati.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Doto Biteko katika mazungumzo yake na Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Ibrahim Uwizeye aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
"Rais Samia ni kinara katika kujenga mahusiano na ndani ya nchi na kimataifa, kama ilivyo kwa uhusiano kati yetu na Burundi ambayo imewezesha kutekeleza miradi kadhaa ukiwemo mradi wa umeme wa RUSUMO unaoendeshwa kwa ubia wa nchi Tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania" amesema Dk. Biteko.
Ameongeza kuwa, Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Burundi na kuwataka kuimarisha mahusiano kwa wafanyabiashara ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Uwizeye amemshukuru Rais Samia kwa utayari wa kuisaidia nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo nishati.
Aidha, Dk. Biteko pia amekutana na Waziri wa Nishati wa Malawi na ujumbe wake, Waziri wa Nishati wa Tunisia, Waziri wa Nishati wa Rwanda, Waziri wa Nishati wa Comoro na Rais wa kampuni ya GE VERNIVA ambao kwa nyakati tofauti wamezungumzia maaendeleo na ushirikiano katika sekta ya nishati.
Mazungumzo haya yamekuja ikiwa ni siku moja baada ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaojulikana kama misheni 300 unaolenga kuwawezesha waafrika milioni 300 barani Afrika kunufaika na nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED