Maswi adai Samia Legal Aid, ni ya wanyonge

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:57 PM Jan 29 2025
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi.
Picha: Mtandao
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, lengo lake kuu ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, hasa kwa wananchi wanyonge.

Maswi, alikuwa akizungumza leo, Januari 29, 2025 katika mkoani Kilimanjaro, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, uliofanyika viwanja vya stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Moshi Mjini. 

Amesema katika kipindi cha utekelezaji wa kampeni hiyo, kazi kubwa zitakazofanyika ni kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kisheria, utawala bora, elimu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, usimamizi wa mirathi na urithi, haki za ardhi na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, haki za binadamu na wajibu yakiwemo pia masuala ya ndoa. 

Amesema kazi zingine ni  kutoa ushauri nasihi na huduma za kisaikolojia kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia, kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwenye sehemu za vizuizi kama magerezani na katika vituo vya polisi, sehemu zenye mikusanyiko kama sokoni, minadani, shuleni na vyuoni. 

Akitoa salamu zake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi amesema: “Wosia ndio namna pekee ya wewe ukifariki dunia kuendelea kuzungumza na kuelekeza namna unavyotaka mali zako zisimamiwe, unapokufa kibubu wajinga wote kwenye ukoo wako watakuja kunyang’anya mali za familia yako. 

…Huduma ya msaada wa kisheria, ni ibada kwa sababu ni suala la kushughulika na maisha ya watu ya kila siku, hivyo ni wakati wa kuifanya kazi hiyo kwa unyeyekevu na ukamilifu wake." 

Katika hotuba yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, ametangaza kuchukuliwa hatua kali kwa watu wote wanaokiuka sheria, haki za binadamu, wanaonyang'anya watu haki za mirathi, wanaosababisha migogoro ya ardhi pamoja na wanaoendeleza ukatili wa kijinsia. 

Amesema katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Kilimanjaro, kipaumbele kikuu ni utoaji wa elimu ya kisheria. 

Kuhusu kampeni hiyo, Dk Ndumbaro, amesema kampeni hiyo ni matokeo ya maono aliyokuwa nayo Rais Dk. Samia, baada ya kubaini ya kuwa watu wengi wana kiu ya haki, jambo ambalo amesema linadhibitishwa na umati mkubwa wa watu wanaojitokeza kwenda kupata ushauri wa kisheria kila mahali kampeni hiyo inapofanyika hapa nchini. 

“Serikali ya awamu ya sita iligundua ya kuwa wananchi wengi na wana kiu ya haki na ndipo Rais Dk. Samia kupitia busara zake akaanzisha kampeni hii nchi nzima ili kukidhi kiu ya haki waliyonayo watu wengi haswa wale ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za wataalam wa kisheria”, amesema. 

Dk. Ndumbaro aliwapaongeza wale wote ambao wamejitokeza kupata huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo jambo ambalo alisema limedhihirisha ustaarabu wa Watanzania wa kutafuta haki kupitia ngazi za kisheria badala ya kuitafuta kupitia maandamano kama ilivyo kwenye maeneo mengine duniani. 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kampeni hiyo ni muhimu kwa wananchi, yenye faida kubwa  na kwamba imekuja wakati muafaka mkoani humo kutokana na ukweli kwamba watu wengi wana kiu na wengi wao hawana uwezo wa kugharamia huduma za kisheria. 

Awali, akiongea kwa niaba ya watakaotoa huduma za kisheria wakati wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa taasisi ya ushauri wa kisheria mkoani Kilimanjaro ya KWIECO Wakili Bi Elizabeth Minde, alimpongeza Rais Dk Samia kwa kuja na wazo la kambi hiyo ya msaada wa kisheria. 

“Kampeni hii imeakisi uwezo na maono chanya aliyonayo Rais Dk Samia; itakuwa ya msaada mkubwa kwa wananchi wengi haswa wakiwemo wale ambao wako maeneo ya vijijini na ambao kwa sababu moja au nyingine hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama kwa ajili ya kupata huduma za kisheria”, amesema Wakili Minde.