MKUU wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Emmanuela Kaganda ameamuru wakazi wa kijiji cha Kiru Dick waliovunja daraja na kuvamia shamba la mwekezaji kujisalimisha ofisini kwake na kuonya watakaokiuka watachukuliwa hatua kali.
Alitoa amri hiyo jana baada ya baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kudaiwa kuvamia eneo la shamba la mwekezaji huyo wa Kampuni ya Amiry Estate kinyume cha sheria.
“Ni makosa kuvamia mashamba ambayo hawayamiliki kisheria.Tuweke maslahi yetu pembeni, masilahi ya taifa mbele, tuanze kutengeneza ukurasa mpya tujenge Kiru yetu,” alisema Kaganda.
Aliwataka wakazi hao wanaodaiwa kuvamia shamba hilo lililoko katika kijiji hicho kuacha mara moja kwa kuwa nchi inahitaji wawekezaji kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Vilevile, aliwasihi wakazi wa kijiji hicho kuishi kwa upendo amani na ushirikiano baina yao na wawekezaji ili kuleta maendeleo kwao na taifa.
Kwa upande wa wakazi hao, wameomba msamaha kwa kosa la kuvamia shamba hilo kwa madai ya kukosa uelewa.
Wakazi hao waliomba msamaha huo baada ya mkuu huyo wa wilaya kuwasomea barua kutoka serikali kuu kuhusu uhalali wa kampuni hiyo kuwekeza kwenye eneo hilo.
Mmoja wa wakulima wa eneo hilo, Omary Hassan, alisema uelewa mdogo wa baadhi yao umesababisha kutokea kwa tukio hilo.
"Wengi wao hawakutambua kuwa mwekezaji yupo kwa nyaraka halali, hivyo wengine kwa kutokutambua wakafanya tukio hilo," alisema Hassan.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED