Tanzania, Burundi kutekeleza mradi wa reli ya kisasa Uvinza, Musongati

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:10 AM Jan 30 2025
Mkurugenzi Shirika la Reli Tanzania(TRC), Masanja Kadogosa (katikati kulia) na Waziri wa Miundombinu Burundi Capt.Diudone Dukundane wakisaini mkataba wa ujenzi wa reli Uvinza-Burundi
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Shirika la Reli Tanzania(TRC), Masanja Kadogosa (katikati kulia) na Waziri wa Miundombinu Burundi Capt.Diudone Dukundane wakisaini mkataba wa ujenzi wa reli Uvinza-Burundi

TANZANIA na Burundi, zimeingia makubaliano ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza hadi Musongati, yenye urefu wa kilomita 282 itakayogharimu dola bilioni 2.154 sawa na Sh. trilion 5.6.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza katika hafla utiaji saini jana, jijini Dar es Salaam, alisema mradi huo una jumla ya vipande viwili, kutoka Uvinza-Malagalasi chenye urefu wa kilomita 180 na Malagalasi-Msongati, chenye urefu wa kilomita 102.

Prof. Mbarawa alitoa maagizo kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unafuata viwango vya kimataifa na wasimamie fedha za mradi zitumike vizuri.

Pia, aliitaka TRC kuwa  ushirikishaji kwa jamii katika ujenzi wa mradi huo, ikiwamo kutoa fursa za ajira kwa wananchi kwenye maeneo ya mradi, ili Watanzania wabadilishe maisha na kuinua uchumi wao kupitia mradi huo.

Alisema ajenda ya Umoja wa Afrika (AU), ifikapo mwaka 2026 nchi za kiafrika kuunganishwa kwa reli za kisasa, hivyo Tanzania inategemewa kwa kiwango kikubwa kuungaisha nchi hizo.

Waziri wa Miundombinu Burundi, Kapteni Diuodone Dukundane, alisema hatua hiyo iliyochukuliwa na marais wawili wa nchi hizo mbili, Tanzania na Burundi, utaweza kuimarisha urafiki wa kudumu na kupanua biashara na kukuza uchumi.

“Tunaishukuru sana serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa, kwani bila yeye sisi tusingefikiwa na reli hii ya kisasa na leo hii, tunatia saini tumetimiza ahadi yetu na sisi kufikiwa na reli hii ya kisasa,” alisema.

Tanzani, Burundi kujenga reli ya kisasa
Aidha alisema mradi huo utakaoenda kuanza utakuwa mfano wa kuigwa, kwa mataifa mengine kwa kuwa, imeonesha nchi za Afrika zikijiunga zitafika mbali.

Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba, alisema fedha za kutekeleza mradi huo ziko tayari na zinasubiri mkandarasi apatikane, ili ujenzi uendelee.

Alisema kwa juhudi na ubunifu za marais wawili wa Tanzania na Burundi, ni kiwango cha juu na kupata fedha za kutekeleza mradi kupitia Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), kwa mara ya kwanza wamewekeza kwenye reli.

Alifafanua, ili ilete tija inatakiwa ikamilike na kuleta ufanisi bila kusita, hivyo vipande ambavyo bado havijakamilika, ikiwamo cha Tabora, Mwanza kwenda Kigoma, vyote vitakamilika sambamba na ujenzi wa reli Tanzania hadi Burundi.

Mkurugenzi Mkuu TRC, Masanja Kadogosa, alisema, ujenzi wa reli hiyo, Uvinza-Burundi utachukua takribani miezi 72 kukamilika, ikiambatana na madaraja ya kuunganisha nchi hizo mbili na magati ya mizigo.

“Tutahakikisha tutatekeleza ukamilikaji wa miundombinu kwa kiwango cha juu, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, kwa thamani ya fedha  na awamu ya pili ya ujenzi unakwenda kukamilika utekelezaji unaendelea Tabora-Kigoma,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Miundombinu, Moshi Kakoso, alisema kamati ilikuwa inakitilia mkazo na kushauri kukamilika kwa uanzishwaji wa mradi hu.

Aidha, tunashauri mradi wa kutoka Dodoma-Makotopola kwenda Tabora-Kigoma, uende sambamba na ujenzi wa mradi kutoka Uvinza-Msingati, ili kiwe kichocheo cha kukuza uchumi kwa wananchi.

Tanzania, Burundi kujenga reli ya kisasa